Mji wa Minneapolis nchini Marekani umegubikwa na simanzi kufuatia shambulio la kinyama lililotokea katika kanisa la shule moja ya Kikatoliki, ambapo mtu mwenye silaha aliwaua watoto wawili na kujeruhi wengine 17. Mamlaka za uchunguzi nchini humo zimegundua kuwa silaha na magazeti ya risasi ya mshambuliaji huyo yalikuwa yameandikwa jumbe mbalimbali za chuki.
Tukio hilo la kutisha lilitokea wakati wanafunzi walipokuwa wamekusanyika kanisani kwa ajili ya misa maalum ya kuadhimisha kuanza kwa muhula mpya wa masomo. Mshambuliaji alianza kwa kufyatua risasi kupitia madirisha ya kanisa kabla ya kuingia ndani na kuendelea kuwamiminia risasi waumini waliokuwemo.
Mkuu wa Idara ya Usalama wa Ndani, Kristi Noem, alithibitisha kupitia mtandao wa X (zamani Twitter) kwamba muuaji huyo alikuwa ameandika maneno ya kutisha kwenye magazeti yake ya risasi, yakiwemo "Kwa ajili ya watoto," "Mungu wako yuko wapi," na "Muueni Donald Trump."
Mshambuliaji ametambuliwa na Mkurugenzi wa Shirika la Upelelezi la FBI, Cathy Pattel, kama Robin Westman, mwanaume mwenye umri wa miaka 23 ambaye inadaiwa alijitambulisha kama mtu aliyebadili jinsia. FBI imelitaja tukio hili kama kitendo cha kigaidi cha ndani na uhalifu wa chuki unaolenga moja kwa moja waumini wa Kanisa Katoliki.
Kamanda wa Polisi wa Minneapolis, Brian O'Hara, alieleza kuwa jumbe hizo pia zilionekana kwenye video ya "ilani" ambayo Westman aliichapisha kwenye mtandao wa YouTube muda mfupi kabla ya kufanya shambulio. Video hiyo iliondolewa baadaye, lakini wachunguzi wanaichambua ili kubaini chanzo hasa cha kitendo hicho.
Katika shambulio hilo, watoto wawili, wenye umri wa miaka 8 na 10, walipoteza maisha. Watu wengine 17 walijeruhiwa, wakiwemo watoto 14 wenye umri kati ya miaka 6 na 14, pamoja na watu wazima watatu wenye umri wa miaka 80. Hata hivyo, Kamanda O'Hara alitoa matumaini kuwa majeruhi wote wanatarajiwa kupona.
Uchunguzi wa awali umebaini kuwa Westman hakuwa na rekodi yoyote ya uhalifu na inaonekana alitekeleza shambulio hilo peke yake. Aidha, bunduki aina ya ‘rifle’, ‘shotgun’, na bastola alizotumia zote zilinunuliwa kihalali hivi karibuni. Baada ya kutekeleza unyama huo, mshambuliaji alijiua nyuma ya jengo la kanisa.