Hali ya usalama nchini Iran imeingia doa kubwa na kuchafuka ghafla huku kile kilichoanza kama kilio cha njaa na ugumu wa maisha kikigeuka kuwa uwanja wa mapambano ya umwagaji damu. Katika kile kinachodhihirisha msemo wa wahenga kuwa "Mwenye njaa hanaiko," maandamano makubwa ya kupinga kuporomoka kwa thamani ya sarafu na kupanda kwa gharama za maisha yamesababisha vifo vya takriban watu sita baada ya nguvu ya dola kutumika kuzima ghasia hizo.
Taarifa kutoka mashirika ya habari ya ndani ya Iran, likiwemo shirika la Fars, zimethibitisha kuwa miji kadhaa imegubikwa na moshi wa matairi na milio ya risasi. Katika mji wa Lordegan uliopo Kusini-Magharibi mwa nchi hiyo, "patashika nguo kuchanika" ilitokea wakati polisi walipojaribu kuwakamata vinara wa maandamano hayo. Katika purukushani hizo, watu wawili wamepoteza maisha huku wengine kadhaa wakijeruhiwa vibaya.
Hasira za wananchi zimeonekana kuvuka mipaka ya uvumilivu, ambapo waandamanaji waliamua kuchoma moto ofisi ya Gavana, mahakama, na majengo ya benki, wakilalamikia mifumo ya fedha inayowakandamiza. Imeelezwa kuwa baadhi ya waandamanaji walikuwa na silaha na kuwashambulia polisi, jambo lililozidisha chuki na uhasama.
Machafuko hayo hayakuishia hapo. Katika mji wa magharibi wa Azna, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya kundi la watu kuvamia Makao Makuu ya Polisi. Katika makabiliano hayo makali, watu watatu walipoteza maisha na wengine 17 kujeruhiwa. Hii ni ishara tosha kuwa wananchi wamechoshwa na hali ya uchumi na wako tayari kupambana na vyombo vya dola uso kwa uso.
Upande wa serikali nao umepata pigo. Shirika la habari la Tasnim limeripoti kuwa mwananamgambo mmoja wa kikosi cha Basij (ambacho kiko chini ya Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu - IRGC) ameuawa huko Kuhdasht, mkoa wa Lorestan, huku askari wengine 13 wakijeruhiwa vibaya. Hii inaashiria kuwa maandamano haya si ya kawaida, bali ni mpambano kamili kati ya raia na dola.
Chanzo cha yote haya ni uchumi. Iran imekuwa ikikabiliwa na "ufukara wa kutupwa" kutokana na vikwazo vya muda mrefu kutoka mataifa ya Magharibi (hususan Marekani na Ulaya) kwa sababu ya miradi yake ya nyuklia na makombora. Vikwazo hivi vimeua thamani ya sarafu ya Iran (Rial), na kusababisha mfumuko wa bei ambao umewafanya wananchi wa kawaida kushindwa kumudu hata bidhaa muhimu. Hivi karibuni, Gavana wa Benki Kuu alitumbuliwa kutokana na kushindwa kudhibiti anguko hilo la sarafu, lakini hatua hiyo haijasaidia kutuliza hasira za "walalahoi".
Licha ya kutumia nguvu kuzima maandamano, serikali ya Iran inaonekana kusoma alama za nyakati na kuhofia nguvu ya umma. Msemaji wa Serikali, Fatemeh Mohajerani, kupitia mtandao wa kijamii wa X (zamani Twitter), ametangaza kuwa Rais amekutana na wawakilishi wa wafanyabiashara na kuahidi mazungumzo. "Mazungumzo ndiyo njia pekee ya kupata ufumbuzi sahihi," aliandika, akijaribu kupunguza joto la kisiasa.
Maandamano haya yaliyoanza jijini Tehran yakiongozwa na wafanyabiashara na baadaye kuungwa mkono na wanafunzi, sasa yanasambaa kwa kasi kama moto wa nyika. Wakati serikali ikijaribu kuzima moto huu kwa mkono mmoja huku mkono mwingine ukiuliza "tufanyeje?", dunia inatazama kwa umakini kuona ikiwa utawala wa Iran utaweza kuhimili mawimbi haya ya njaa na kiu ya mabadiliko ya kiuchumi.