Mji wa Chizhou, katika jimbo la Anhui nchini China, umeshuhudia tukio la kushtua ambapo sehemu kubwa ya vigae vya paa la jengo la kihistoria la 'Mingzhong Drum Tower' lililoanzia enzi ya Ming, limeporomoka. Tukio hili lilitokea majira ya saa 12 na nusu jioni kwa saa za huko, na kusababisha taharuki kwa wananchi waliokuwa karibu, ambao walifanikiwa kukimbia na hivyo kuepuka majeraha.
Video zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii zilionyesha wingu kubwa la vumbi likifuka huku vigae vikishuka kwa kasi kutoka sehemu ya juu ya ghorofa hilo, kama vile tsunami ya matofali. Sauti ya mtu ikisema "vigae vinaanguka!" ilisikika, ikionyesha jinsi watu walivyoharakisha kuondoka eneo hilo. Vigae viliendelea kuanguka kwa muda wa dakika moja hadi mbili.
Mara baada ya tukio hilo, maafisa wa idara ya urithi wa kitamaduni wa eneo hilo walifika mara moja kwenye eneo la tukio. Waliweka uzio wa usalama na kuanza uchunguzi wa haraka. Ofisi ya Utamaduni na Utalii ya Wilaya ya Pingyang, ambako ghorofa hilo linapatikana, imeahidi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini chanzo halisi cha ajali hiyo, ikiwa ni pamoja na uwezekano wa ujenzi duni. Hadi uchunguzi utakapokamilika na ukarabati kufanyika, ghorofa la Mingzhong Drum Tower limefungwa kwa umma.
Katika taarifa rasmi, Ofisi ya Utamaduni na Utalii ya Pingyang ilithibitisha kuanguka kwa sehemu ya paa la ghorofa hilo lililojengwa upya mwaka 1995, na kusema kuwa hakuna mtu aliyejeruhiwa. Waliongeza kuwa sababu ya tukio hilo bado inachunguzwa.
Ghorofa la Mingzhong Drum Tower ni moja ya majengo makubwa zaidi ya aina yake nchini China yaliyopo hadi sasa. Lina historia ndefu, likiwa limejengwa mwaka 1375 katika Wilaya ya Pingyang wakati wa utawala wa Kaisari Zhu Yuanzhang, mwanzilishi wa nasaba ya Ming, ambaye alikuwa na mipango ya kuhamisha mji mkuu. Katika kipindi cha nasaba ya Qing, sehemu zote za jengo hilo ziliharibiwa isipokuwa msingi wake wa mawe. Jengo lililopo sasa lilijengwa upya mwaka 1995.
Ghorofa hilo lilikuwa linatumika kama makumbusho ya kumuenzi Zhu Yuanzhang na kuelezea historia ya awali ya nasaba ya Ming. Hata hivyo, tangu mwaka 2017, kumekuwa na matukio ya mara kwa mara ya vigae kuanguka na uharibifu wa sehemu za juu za paa. Kutokana na hali hiyo, mnamo Septemba 2023, serikali ilitumia Yuan milioni 3.4 (takriban Shilingi za Kitanzania Bilioni 1.5) kwa ajili ya ukarabati, ambao ulikamilika Machi 2024.
Lakini, miezi 15 tu baada ya ukarabati huo, sehemu kubwa ya vigae imeanguka, jambo ambalo limezua hasira na shutuma dhidi ya uwezekano wa ujenzi duni na matumizi mabaya ya fedha za umma.
Huku kukiwa na malalamiko hayo, Mkurugenzi wa Ofisi ya Utamaduni na Utalii ya Pingyang, Bw. Lu Deyong, alitoa kauli ambayo iliongeza hasira za wananchi. Alisema kuwa jengo hilo lililojengwa upya mwaka 1995 "lilikuwa jengo haramu" kwani halikupata idhini kutoka kwa Ofisi ya Urithi wa Utamaduni ya Jimbo la Anhui. Aliongeza kuwa msingi wa jengo hilo ni urithi wa kitamaduni, lakini sehemu ya juu siyo. Kauli hii ilionekana kama kujaribu kukwepa lawama na badala yake ilikasirisha zaidi umma. Tukio hili linaibua maswali mengi kuhusu ubora wa kazi za ukarabati na usimamizi wa majengo ya kihistoria nchini China.