Kaimu Mtendaji Mkuu wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Anita Mendoza, alimkabidhi fomu ya kugombea uenyekiti mtia nia, Deodatus Balile.
Balile aliingia madarakani mwaka 2016 baada ya kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti, na mwaka 2018 Mwenyekiti aliyekuwepo alijiuzulu ndipo alikaimu nafasi ya Mwenyekiti.
Aidha, Mei 21, mwaka 2021, TEF ilifanya Uchaguzi Mkuu mjini Morogoro ambapo aliibuka mshindi na kuongoza kwa miaka minne inayokwisha sasa.
"Nilichaguliwa kipindi cha kwanza cha miaka minne na sasa nawaomba wahariri wenzangu kuwaongoza kwa kipindi kingine cha mwisho," amesema.
"Kinachonisukuma kuendelea kugombea nafasi hii ni kutetea mabadiliko kwenye mfumo wa sekta ya habari na uchumi wa vyombo vya habari nchini," amesema na kuongeza;
"Uzoefu wangu wa miaka mingi kwenye sekta ya habari umenifanya nifahamu mbinu nyingi za kuikwamua sekta hii, hasa kwenye uchumi wa vyombo vya habari katika kipindi chenye changamoto nyingi ikiwamo za uwepo wa dijitali," amesema.
Aidha, amesema ameshajenga misingi ya uandishi wa habari nchini, na kwamba sasa ni kujenga nyumba halisi yenye kutoa taswira nzuri kwa tasnia hiyo ambayo ni muhimili wa nne usio rasmi.
Wenyeviti waliopita TEF ni Absalom Kibanda na Theophil Makunga.
Mkutano Mkuu Maalum wenye agenda moja ya uchaguzi mkuu utafanyika mjini Songea, mkoani Ruvuma na kuwaleta pamoja wahariri zaidi ya 200 kutoka maeneo mbalimbali nchini.