Hatimaye, Rais wa Kenya, William Ruto, amewateua rasmi Mwenyekiti na Makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), hatua inayomaliza mkwamo wa muda mrefu uliosababishwa na vita vya kisheria mahakamani. Uteuzi huu unafungua rasmi safari ya maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao nchini humo.
Kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali namba 9269, la Julai 10, 2025, Rais Ruto amemteua Erastus Edung Ethekon kuwa Mwenyekiti mpya wa IEBC kwa kipindi cha miaka sita.
Katika tangazo lingine (Namba 9270), Rais Ruto pia aliwateua watu sita kuwa Makamishna wa tume hiyo muhimu. Wateule hao ni Ann Njeri Nderitu, Moses Alutalala Mukhwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor Hassan, Francis Odhiambo Aduol, na Fahima Araphat Abdallah.
Uteuzi huu umekuja baada ya jopo la majaji watatu wa Mahakama Kuu kutupilia mbali kesi iliyokuwa imefunguliwa kupinga uhalali wa mchakato huo. Hata hivyo, mahakama ilibaini kuwa tangazo la awali la uteuzi lilikuwa limechapishwa kinyume na amri ya mahakama iliyokuwa imezuia hatua hiyo kwa muda.
Kutokana na hitilafu hiyo ya kiutaratibu, mahakama ilibatilisha tangazo la awali na kuamuru Rais atoe matangazo mapya, jambo ambalo sasa limetekelezwa kwa mujibu wa sheria.
Kufuatia kuchapishwa kwa matangazo haya mapya na halali, Mwenyekiti na Makamishna hao wapya sasa wanatarajiwa kula kiapo mbele ya Jaji Mkuu wa Kenya ili waweze kuanza rasmi majukumu yao ya kusimamia chaguzi nchini humo.