TANROADS Kagera Yajipanga Kukabiliana na Athari za Mvua kwa Masaa 24

economy | Sat Apr 12 2025


TANROADS Kagera Yajipanga Kukabiliana na Athari za Mvua kwa Masaa 24

Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kagera umeweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha, kuhakikisha usalama wa barabara unarejeshwa ndani ya saa 24 katika mkoa huo.


Meneja wa wakala huo mkoani Kagera, Bwana Ntuli Mwaikosesya, amesema kuwa kutokana na mvua kubwa iliyoanza kunyesha mwezi Machi mwaka huu, timu ya wataalamu wa ufundi kutoka ofisi yake imejipanga kikamilifu kukabiliana na athari zote zinazoweza kujitokeza.


Alisema kuwa miongoni mwa barabara ambazo ziliathirika awali ni barabara ya Kasozibakaya – Kabindi – Nyantakara yenye urefu wa kilometa 82, ambayo iliharibika sehemu ndogo. Hata hivyo, alieleza kuwa madhara hayo yalishughulikiwa ndani ya saa 24 na sasa barabara hiyo inapitika vizuri, hivyo kuruhusu wananchi kuendelea kupata huduma zote muhimu.


"TANROADS tunasimamia mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa 2072 katika mkoa wa Kagera, na kwa sasa barabara zote zinapitika vizuri. Hii ni kwa sababu tuna vifaa, mitambo, wahandisi, na wakandarasi ambao wako tayari kwa dharura yoyote ile ambayo inaweza kujitokeza wakati wa mvua. Lengo letu ni kuhakikisha wananchi hawakwami katika kupata huduma zote wanazohitaji, tukizingatia kuwa tunaungana na nchi za Afrika Mashariki, hivyo tuko tayari kukabiliana na madhara yoyote ya mvua," alisisitiza Bwana Mwaikosesya.


Aliongeza kuwa athari za mvua ya El Nino zilizosababisha uharibifu mkubwa kwa barabara katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Kagera tayari zimeshafanyiwa matengenezo kwa gharama ya Shilingi bilioni 4.6 za Kitanzania.


"Barabara ya Nyabihanga – Minziro, Mutukula – Bukoba, Bugene – Kaisho, na Rutenge – Kishoju zimekamilika kwa asilimia 100, na wananchi wanaendelea kupata huduma kupitia barabara hizo," alisema.


Bwana Mwaikosesya alitoa wito kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wanapoona maji yakikatiza kwa kasi kwenye barabara na madaraja. Pia, aliwashauri kupunguza shughuli za kilimo karibu na kingo za barabara, kuacha tabia ya kuiba alama za barabarani, na kuacha kutupa taka chini ya makalavati kwani tabia hizo zinasababisha mitaro kuziba na kushindwa kupitisha maji.


TANROADS Mkoa wa Kagera imetenga bajeti ya Shilingi bilioni 12 kwa mwaka wa fedha 2024/2025 kwa ajili ya matengenezo ya kawaida ya barabara, hatua ambayo inawezesha wakala kukabiliana na dharura zozote zinazoweza kujitokeza wakati wowote.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.