Serikali imetoa pongezi zake kwa Taasisi ya NMB Foundation kwa kuendesha mafunzo muhimu kwa wakulima wa zao la kakao kutoka Vyama vya Msingi vya Ushirika wa Kilimo na Masoko (AMCOS) katika wilaya ya Kyela, mkoani Mbeya. Serikali imebainisha kuwa hatua hiyo iliyochukuliwa na taasisi hiyo ni wazi inaunga mkono kikamilifu juhudi zinazoendeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuinua sekta ya kilimo na kuboresha maisha ya wakulima nchini.
Mafunzo hayo, yaliyolenga kuongeza thamani ya zao la kakao, masoko, na uandaaji wa mipango biashara, yamefanyika kwa muda wa siku nne na kuhusisha washiriki 74 kutoka AMCOS 37 tofauti. Hafla ya kufunga mafunzo hayo ilifanywa na Mkuu wa Wilaya ya Kyela, Bi. Josephine Manase, ambaye alitoa vyeti kwa washiriki waliohudhuria.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo ya kufunga mafunzo, DC Manase aliipongeza sana NMB Foundation na Rabo Foundation kwa kushirikiana na Chama Kikuu cha Ushirika wa Kilimo na Masoko Kyela (KYECU) kufanikisha mafunzo haya muhimu kwa wadau wote wanaohusika katika mnyororo wa thamani wa zao la kakao. Alisema ushirikiano huu unasaidia kwa kiasi kikubwa jitihada za serikali katika kuinua sekta hii muhimu.
“Ninaposimama hapa kufunga mafunzo haya, basi nianze kwa kuipongeza NMB Foundation na washirika wao Rabo Foundation kwa mafunzo haya, ambayo yanaonyesha dhamira yenu ya dhati ya kuliongezea thamani zao la kakao wilayani Kyela na kukuza uchumi wa wakulima na wadau wake wote,” alisema DC Manase.
Alikumbusha kuwa katika hotuba zake nyingi, Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa akisifu ubora wa kakao inayozalishwa Kyela, na kile ambacho NMB Foundation wamekifanya kinaenda sambamba na juhudi za Serikali Kuu na Serikali ya Wilaya ya Kyela katika kuongeza thamani ya zao hili, ambalo limekuwa na mchango mkubwa katika uchumi wa taifa.
Mkuu wa Wilaya alitoa wito kwa NMB Foundation na washirika wake kuhakikisha kuwa elimu iliyotolewa haishii tu darasani, bali inaakisiwa katika kazi za kila siku za mamia na maelfu ya wanachama wa AMCOS waliowawakilisha. Alisisitiza umuhimu wa kufanikisha mada zilizofundishwa, ikiwemo ile ya uchakataji wa kakao, ili kuharakisha ukuaji wa uchumi wa wakulima.
Bi. Manase alibainisha kuwa mafunzo hayo, iwapo yatatumiwa vizuri, yatakuwa chombo muhimu katika kubadilisha maisha na kukuza uchumi wa wakulima katika wilaya yake, hasa kutokana na aina ya mada zilizotolewa na wakufunzi kutoka NMB Foundation na Rabo Foundation. Alieleza kuwa kupitia mafunzo hayo, wakulima wamejifunza mbinu za kuboresha zao la kakao ili kukidhi mahitaji ya soko la uhakika, kuongeza mapato kupitia uuzaji wa kakao iliyoboreshwa, kufungua fursa za ajira kwa vijana na wanawake wanaoshiriki katika mnyororo wa thamani wa zao hili, na kupata elimu ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.
Zaidi ya hayo, aliongeza kuwa wakulima wamepata elimu ya fedha na kujua jinsi ya kupata mikopo nafuu kwa ajili ya kuendeleza kilimo chao, pamoja na matumizi sahihi ya mikopo hiyo kwa kununua mahitaji muhimu ya zao husika na kukuza uzalishaji. Alisisitiza kuwa juhudi hizi za NMB Foundation zinapaswa kuigwa na kuendelezwa na taasisi nyingine.
Kwa upande wake, Mratibu wa NMB Foundation Kanda ya Nyanda za Juu, Rodgers Shipella, alisema kuwa taasisi yake kwa kushirikiana na Rabo Foundation, wameanzisha na kutekeleza mradi wa kuongeza thamani ya zao la kakao kwa kuwajengea uwezo wakulima kupitia ushirika katika maeneo mbalimbali. Alitaja maeneo hayo kuwa ni elimu ya ushirika, uongozi bora ndani ya ushirika, ujasiriamali, elimu ya fedha na usimamizi wa mikopo, kuongeza thamani ya zao, uhakika wa masoko ili kuongeza uzalishaji na uchakataji wa kakao katika wilaya ya Kyela.
Shipella alieleza kuwa NMB Foundation ilianza rasmi kutekeleza mradi huu Oktoba 2023, na hadi sasa wameweza kuwafikia wakulima 1,281, wakiwemo wanawake 314 na wanaume 967. Lengo kuu la mradi huu sio tu kuongeza thamani ya zao la kakao, bali pia kuweka uwiano sahihi wa bei. Aliongeza kuwa mradi huo unalenga pia kuibua ajira za uchakataji wa kakao kwa vijana na wanawake, ili kuwapanulia fursa za kujiongezea kipato cha kila siku. Alisisitiza kuwa mradi huu utawanufaisha wakulima na vyama vyao, pamoja na wadau wengine kama vile ushirika, serikali, na wanunuzi.
Akifafanua zaidi, Shipella alisema kuwa mkulima atapata bei bora na yenye uwiano, uhakika wa soko, kuongeza ari na hamasa ya uboreshaji wa kakao na kuongeza kipato. Serikali za mitaa na serikali kuu nazo zitanufaika kwa kuongeza mapato, kukuza na kuendeleza uzalishaji wa zao hilo, kupitia kodi ya ongezeko la thamani (VAT), PAYE, na ajira kwa vijana na wanawake.
Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Wilaya ya Kyela (KYECU Ltd), Nabii Emmanuel Mwakyenda, aliishukuru NMB Foundation kwa kuwapa mafunzo muhimu wanachama wa AMCOS 37 za wilaya yake, akieleza imani yake kuwa mafunzo na elimu waliyopata yatakuwa chachu ya ustawi na uendelevu wa zao la kakao wilayani humo.
Akisoma risala kwa niaba ya washiriki, Evance Mwaipopo kutoka Mwabusye AMCOS, aliipongeza NMB Foundation kwa uendeshaji mzuri wa mafunzo, ambayo yamewanufaisha kupitia mada mbalimbali zikiwemo za uongezaji thamani wa kakao, kilimo cha kakao bila kukata miti, ujasiriamali, na mpango biashara. Washiriki waliomba NMB Foundation kuendelea kuwajali na kuwathamini wakulima wa kakao Kyela, huku wakiitaka serikali kwa upande wake kuzipa kipaumbele barabara zinazoingia na kutoka Kyela, ambazo ni chakavu, ili kurahisisha usafirishaji wa mazao mbalimbali, ikiwemo kakao.