Timu maalum ya ufuatiliaji iliyoundwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara imekutana na wadau mbalimbali wa sekta ya viwanda katika mkoa wa Tanga. Hatua hii ni sehemu ya utekelezaji wa agizo lililotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan la kuifanya Tanga kuwa mkoa wa viwanda kama ilivyokuwa zamani.
Wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Tanga hivi karibuni, Rais Samia alieleza kuwa moja ya malengo yake makubwa katika kuongoza Tanzania ni kuifufua Tanga na kuirejesha katika hadhi yake ya kuwa mkoa wa viwanda, eneo ambalo lilikuwa na viwanda vingi na vilivyokuwa vikichangia sana katika uchumi wa nchi.
Akizungumza katika kikao hicho na wadau, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda na Biashara, Bwana Juma Mwambapa, alisema kuwa juhudi za kuirejesha Tanga kuwa mkoa wa viwanda ni sehemu muhimu ya mkakati wa serikali katika kuimarisha uchumi wa viwanda nchini na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.
"Tanga inakwenda kuwa kitovu cha viwanda nchini, hivyo kwa kushirikiana kwa karibu na wadau wote muhimu, tunakwenda kurudisha hadhi hiyo na hivyo kufungua fursa nyingi za ajira kwa vijana wetu, lakini pia kuimarisha uchumi wa mkoa huu," alisema Mwambapa.
Aidha, alieleza kuwa uboreshaji wa miundombinu muhimu kama bandari ya Tanga, reli, na barabara, utawezesha sana kuimarika kwa uchumi wa viwanda katika mkoa huo. Miundombinu bora ni muhimu ili kuwezesha usafirishaji wa malighafi na bidhaa kutoka na kuingia mkoani Tanga.
"Tunakutana na wadau ili tuweze kubaini changamoto zilizosababisha viwanda kufa na kuweka mazingira rafiki ya kufanikisha uwekezaji wa viwanda vipya, lakini pia kufufua viwanda vilivyokuwepo hapo awali," alibainisha Mwambapa.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Tanga, Bwana Sebastian Masanja, alieleza kuwa uongozi wa mkoa uko tayari kushirikiana kwa karibu na wawekezaji katika kuhakikisha kuwa mazingira mazuri ya uwekezaji yanapatikana. Hii ni pamoja na kutatua changamoto za miundombinu na upatikanaji wa malighafi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara, Wenye Viwanda na Wakulima Tanzania (TCCIA) mkoani Tanga, Bwana Rashid Mwanyoka, alisema kuwa wao kama wadau wakuu wa ajenda hiyo wameiomba serikali kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji. Hii ni pamoja na kubainisha maeneo maalum kwa ajili ya fursa za uwekezaji wa viwanda vikubwa, vya kati, na vidogo.