Kilio cha muda mrefu cha uhaba wa maji kwa zaidi ya wakazi 14,750 wa Kata ya Kwadelo, Wilayani Kondoa, kimefika tamati baada ya Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) kuzindua rasmi mradi mkubwa wa maji safi na salama. Mradi huu wa kihistoria, ulioigharimu kampuni hiyo kiasi cha Shilingi milioni 292, unatarajiwa kubadilisha kabisa maisha ya jamii hiyo kiuchumi na kiafya.
Mradi huu, ambao ni sehemu ya mpango endelevu wa SBL ujulikanao kama "Water of Life", umetekelezwa kwa ushirikiano na shirika la Africa Community Advancement Initiative (Africai). Uwekezaji huo umewezesha ujenzi wa miundombinu ya kisasa, ikiwemo osesho la pampu yenye nguvu (submersible pump), nyumba ya mashine, tanki kubwa la saruji la kuhifadhi maji, na mtandao mpana wa mabomba unaosambaza maji kwenye vituo 11 vya umma. Miundombinu hii ina uwezo wa kuzalisha na kusambaza zaidi ya lita 107,000 za maji kila siku, na hivyo kumaliza adha ya kutafuta maji kwa umbali mrefu.
Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi, alisema mradi huo ni uthibitisho wa dhamira ya kampuni katika kusaidia maendeleo ya jamii. "Tunaamini kwa dhati kuwa upatikanaji wa maji ni msingi wa uhai, heshima, na maendeleo ya kiuchumi. Tunajivunia kuunga mkono juhudi za serikali na kutekeleza miradi inayolingana na malengo yetu ya Mazingira, Jamii na Utawala Bora (ESG) pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050," alisema Anyalebechi. Tangu mwaka 2010, SBL imetekeleza miradi 28 ya maji nchini, ikinufaisha zaidi ya Watanzania milioni mbili.
Mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Mifugo na Uvuvi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Kondoa, Mheshimiwa Dk. Ashatu Kijaji, aliipongeza SBL kwa kuwa mfano bora wa ushirikiano kati ya sekta binafsi na serikali katika kuleta maendeleo. "Serikali inathamini sana mchango wa sekta binafsi kama SBL. Mradi huu sio tu unatoa maji; unarejesha heshima, unalinda afya za wananchi, na unafungua fursa nyingi za kiuchumi, hasa kwa wanawake na watoto," alisisitiza Dk. Kijaji.
SBL imesisitiza kuwa huu ni mwanzo tu na itaendelea kuwekeza katika miradi inayobadilisha maisha ya Watanzania, huku ikitoa wito kwa wadau wengine kushirikiana katika kujenga Tanzania iliyo bora zaidi.