Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa moja ya mafanikio makubwa ya serikali yake ni kuwezesha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa fursa kwa sekta binafsi na watu waliojiajiri kujiwekea akiba kwa ajili ya maisha yao ya baadaye. Hatua hii imewaletea matumaini makubwa Watanzania wengi ambao hapo awali hawakuwa na uhakika wa maisha baada ya kustaafu au kukumbwa na changamoto za kiafya.
Akizungumza katika sherehe za Siku ya Wanawake Duniani zilizofanyika kitaifa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha, Rais Samia alieleza kuwa hatua hii ni sehemu ya juhudi za serikali kuhakikisha wananchi wote wanakuwa na uhakika wa maisha hata wanapostaafu au wanapokumbwa na changamoto za kiafya. "Jambo jingine katika hifadhi ya jamii ni pale tuliporuhusu Mifuko yetu ya Hifadhi ya Jamii itoe madirisha ambayo sekta binafsi na sekta isiyo rasmi nayo itapata ridhaa ya kujiwekea hifadhi," alisema Rais Samia.
Rais Samia alisisitiza kuwa mfumo huu unaendelea kutekelezwa kwa mafanikio, na kwamba hatua hiyo inazidi kuimarisha usalama wa kiuchumi kwa wananchi wote wa Tanzania. Hii ni hatua muhimu katika kujenga uchumi imara na wenye usawa, ambapo kila Mtanzania anahisi ana thamani na ana uhakika wa maisha bora.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, aliipongeza Mamlaka ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii (NSSF) kwa jitihada zake za kutoa elimu kuhusu hifadhi ya jamii kwa wananchi waliojiajiri. Alisema kuwa mfumo huu mpya umeleta matumaini mapya kwa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi ambao hapo awali hawakuwa na uhakika wa kupata pensheni au huduma za matibabu. "NSSF wamefanya kazi kubwa sana, wananchi wa Mkoa wa Arusha sasa wana uhakika wa kuwa na pensheni hata wale ambao si wafanyakazi wa serikali. Mfumo huu ulioundwa na Mheshimiwa Rais Samia ni wa kipekee, unamwezesha mwananchi wa kawaida kuwa na akiba na pia kupata matibabu katika mazingira bora," alisema Makonda.
Elimu hiyo kwa wananchi waliojiajiri imekuwa ikitolewa kupitia kampeni ya ‘NSSF Staa wa Mchezo’, iliyoanzishwa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Ridhiwani Kikwete. Kampeni hii inafanyika maeneo mbalimbali nchini, ikiwa ni juhudi za kuhakikisha kila Mtanzania anapata uelewa wa umuhimu wa hifadhi ya jamii.
Kupitia kampeni hii, wananchi waliojiajiri wanahamasishwa kujiunga na mpango wa ‘Hifadhi Scheme’ kwa kuchangia kiasi kidogo cha pesa kupitia simu kwa kubofya *152*00#. Mwanachama anaweza kuchangia Shilingi 30,000 au zaidi kwa utaratibu unaomfaa, iwe kwa siku, wiki, mwezi, au msimu. Kupitia mpango huu, wanachama wanapata mafao ya matibabu na pensheni ya uzeeni. Kwa mujibu wa NSSF, wanachama wanaweza pia kuchangia Shilingi 52,200 kwa mwaka, kiasi ambacho kinawawezesha wao na wategemezi wao watano (mume/mke na watoto wanne) kupata huduma za matibabu.
Katika Jiji la Arusha, elimu kuhusu mpango huu ilitolewa katika soko la Kilombero, ambapo mamia ya wananchi waliojiajiri walijiunga na NSSF kwa ajili ya kuweka akiba kwa maisha bora ya sasa na ya baadaye. Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, aliongoza kampeni hiyo, akisisitiza kuwa ujio wa ‘Hifadhi Scheme’ unaleta mapinduzi katika mfumo wa hifadhi ya jamii kwa sekta isiyo rasmi.
Mpango wa ‘Hifadhi Scheme’ umelenga watu walioko katika sekta mbalimbali kama vile kilimo, ufugaji, uvuvi, madini (wachimbaji wadogo), usafirishaji (Bodaboda na Bajaji), na biashara ndogo ndogo (Machinga, Mama/Baba Lishe, Wauza mkaa, wauza nyanya, wasusi, na wengine). Kwa mujibu wa NSSF, mpango huu unatoa fursa kwa waliojiajiri kuwa na usalama wa kiuchumi kwa maisha ya baadaye, huku ukihakikisha wanapata huduma muhimu kama matibabu na mafao mengine.
Hatua hii inaifanya NSSF kuwa "Staa wa Mchezo" kwa wananchi waliojiajiri, kwani sasa wanahakikishiwa maisha bora ya sasa na baadaye kupitia huduma mbalimbali za hifadhi ya jamii kwa mujibu wa sheria.