Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) umeandika historia ya mafanikio makubwa, ambapo thamani ya Mfuko imepaa kwa karibu asilimia 100 ndani ya miaka minne, kutoka Shilingi trilioni 4.8 mwaka 2021 hadi kufikia Shilingi trilioni 9.6 mwezi Juni 2025. Ukuaji huu wa kihistoria sasa unawezesha Mfuko kuweka lengo kabambe la kuanza kulipa mafao ya kustaafu ndani ya saa 24 tu.
Akizungumza jana mkoani Singida katika kikao kazi maalum kati ya NSSF na Majaji wa Mahakama ya Rufani, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba, alisema mafanikio hayo yanatokana na mambo makuu matatu: maboresho ya sheria, mazingira wezeshi ya kisera yaliyowekwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na mapinduzi ya kidijitali.
Mshomba alifafanua kuwa mabadiliko ya Sheria ya NSSF ya mwaka 2018 na 2024 yamefungua milango kwa mamilioni ya Watanzania katika sekta binafsi na sekta isiyo rasmi kujiunga na hifadhi ya jamii, jambo lililochangia kuongezeka kwa wanachama kutoka milioni 1.3 hadi zaidi ya milioni 1.8.
"Ongezeko hili la wanachama, pamoja na uwekezaji wenye tija, vimepandisha ukusanyaji wa michango kutoka Shilingi trilioni 1 hadi trilioni 2.16 kwa mwaka," alisema Mshomba. Aliongeza kuwa, "Kupitia maboresho ya TEHAMA, sasa asilimia 90 ya huduma zetu ni za kidijitali, na hii ndiyo inatupa ujasiri wa kuweka lengo la kulipa mafao ya uzeeni ndani ya saa 24 baada ya mwanachama kustaafu."
Akifungua kikao hicho, Jaji wa Mahakama ya Rufani, Augustine Mwarija, alipongeza ushirikiano huo kati ya NSSF na Mahakama, akisema ni muhimu katika kuhakikisha haki za wanachama zinalindwa na changamoto kama za mirathi zinatatuliwa kwa haraka.
"Kikao hiki, kilichoandaliwa kwa ushirikiano na Chama cha Mahakimu na Majaji Tanzania (TMJA), ni jukwaa muhimu la kubadilishana uzoefu ili kuhakikisha wastaafu wanapata haki zao kwa wakati. Tunawapongeza NSSF kwa hatua kubwa wanazopiga," alisema Jaji Mwarija.
Licha ya mafanikio hayo, NSSF ilibainisha bado kuna changamoto ya baadhi ya waajiri kutowasilisha michango kwa wakati, lakini iliahidi kuendelea kutoa elimu ili kuhakikisha kila mfanyakazi anapata haki yake ya kuwa na hifadhi ya jamii.