Baada ya ukimya wa muda mrefu na mabadiliko ya mifumo, hatimaye "Bomba la Pesa" la mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri nchini limefunguka tena, safari hii likipitia katika mifumo rasmi ya kibenki. Hatua hii imepokelewa kwa vifijo na nderemo na wajasiriamali wanawake, vijana, na wenye ulemavu ambao walikuwa wamekata tamaa ya kupata mitaji. Hata hivyo, katikati ya shangwe hizo, kumeibuka kilio cha chini kwa chini kuhusu mzigo mzito wa marejesho ya kila mwezi unaotishia uhai wa biashara zao changa.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wanufaika wa mikopo hiyo wameipongeza Serikali kwa kurejesha utaratibu huo ambao ni mkombozi kwa mwananchi wa kawaida asiye na dhamana za kibenki. Lakini, wametoa rai kwa mamlaka husika kuangalia upya viwango vya marejesho, wakidai kuwa ratiba ya kulipa kati ya Shilingi 200,000 hadi 300,000 kwa mwezi ni "mzigo wa misumari" kwa biashara ambazo bado zinajikongoja kusimama.
Kilinge cha Sheria: Mwarobaini wa Urasimu Imebainika kuwa kikwazo kikubwa kilichokuwa kikiwakwamisha wengi si kukosekana kwa fedha tu, bali ni kutojua "pasipoti" ya kuzifikia fedha hizo. Kutokana na changamoto ya ukosefu wa elimu ya kutosha juu ya maandiko ya miradi na katiba za vikundi, Taasisi ya Women of Influence imeamua kuvaa njuga suala hilo.
Kupitia mradi wao bunifu wa Kilinge cha Sheria, taasisi hiyo imekuwa ikifanya kazi ya ziada kuwarasimisha wanawake kisheria. Wanawasaidia kuandaa nyaraka muhimu, katiba za vikundi, na kupata Namba ya Utambulisho wa Mlipa Kodi (TIN), hatua ambazo ni muhimu ili kukopesheka.
Mmoja wa wanufaika kutoka Kikundi cha Mkombozi, Bi. Silia Alphonce, amekiri kuwa bila msaada huo, wangekwama. "Tunamshukuru Mungu na serikali, lakini pia Kilinge cha Sheria wametutoa gizani. Awali tulitumia muda mwingi kufuatilia bila mafanikio kwa sababu vigezo havikuwa wazi. Tunaiomba serikali iweke mambo hadharani mapema ili tusionekane tunazunguka mbuyu," alisema Silia.
Kilio cha Marejesho na Ushuhuda wa Milioni 39.5 Bi. Zuhura Juma, mnufaika mwingine, ameongeza kuwa licha ya furaha ya kupata mtaji, 'presha' inakuja mwisho wa mwezi. "Tunapata fedha ndiyo, lakini serikali itupunguzie kasi ya marejesho. Biashara zina panda shuka, ukibana sana kwenye marejesho makubwa, unaua mtaji wenyewe," alilalamika Zuhura.
Akifafanua mafanikio ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Women of Influence, Bi. Doreen Kalugira, amebainisha kuwa jitihada zao zimezaa matunda yanayoonekana. Tayari wamefanikiwa kuvivusha vikundi viwili vya Mkombozi na Nange kutoka kata ya Kigogo jijini Dar es Salaam, ambavyo kwa pamoja vimefanikiwa kupata mikopo yenye thamani ya Shilingi Milioni 39.5 kutoka mfuko wa serikali.
Mapinduzi ya Kidijitali: 'Kilinge Digital' Katika kuhakikisha wanawake hawapitwi na wakati, Doreen ameleza kuwa wameanzisha programu ya simu (App) inayoitwa Kilinge Digital. Programu hii inawapa wanawake taarifa sahihi za mikopo rafiki kiganjani mwao, ikilenga kuondoa adha ya kutapeliwa au kukosa taarifa sahihi.
Jitihada hizi zinaungwa mkono na wafadhili wa kimataifa, Women First International ya Marekani, ikilenga si tu kukuza uchumi, bali pia kupambana na ukatili wa kijinsia na rushwa ya ngono ambayo mara nyingi huwanyemelea wanawake wanaposaka mitaji.
Wito umetolewa kwa wanawake kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa hizi, huku serikali ikitakiwa kuboresha mazingira ya marejesho ili mikopo hii iweze kweli kuwa daraja la kutoka kwenye umaskini.