Maelfu ya wananchi wanaotumia barabara ya kusini wamejikuta katika hali ngumu baada ya njia hiyo ya Somanga Mtama kuharibiwa vibaya kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini. Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, ametoa agizo kali kwa wataalamu wa ujenzi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kufanya kazi mchana na usiku ili kuhakikisha huduma za usafiri zinarejea haraka iwezekanavyo.
TANROADS ilikuwa imetoa taarifa saa chache zilizopita kuhusu kufungwa kwa muda kwa barabara hiyo muhimu baada ya kuharibiwa na mvua kubwa zilizosababisha mafuriko makubwa katika Wilaya ya Kilwa. Mafuriko hayo yamesababisha uharibifu mkubwa kwa daraja la muda lililokuwa limejengwa katika eneo hilo, na hivyo kusababisha usumbufu mkubwa kwa wasafiri.
Waziri Ulega, alipofika eneo hilo leo Jumatatu, alitoa salamu za pole kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa wananchi wote waliokwama kutokana na tatizo hilo. Aliwahakikishia kuwa serikali itatoa ulinzi na usalama kwa kipindi chote ambacho wasafiri hao watakuwa wamesimama, sambamba na kuhakikisha upatikanaji wa huduma zote muhimu za kibinadamu.
"Serikali, baada ya kukumbana na tatizo kama hili mwaka jana, ilianza mara moja kufanya kazi muhimu ya kutafuta suluhu ya kudumu. Suluhu hiyo ni ujenzi wa madaraja imara. Kwa barabara hii pekee, tuna madaraja zaidi ya matano yanajengwa. Kwa Mkoa wa Lindi pekee, Rais Samia aliidhinisha jumla ya Shilingi Bilioni 130 kwa ajili ya kujenga madaraja yaliyoharibika," alisema Waziri Ulega.
Alifafanua kuwa daraja lililoharibika kwa sasa ni la muda tu, na ujenzi wa daraja la kudumu umefikia asilimia 48. Aliongeza kuwa nguzo takribani 27 kati ya 48, zenye urefu wa zaidi ya mita 12, zimeshawekwa imara ardhini. Hii inatoa matumaini kuwa suluhu ya kudumu itapatikana hivi karibuni.
Katika hatua nyingine, Waziri Ulega alionesha kukerwa na uzembe uliojitokeza katika kushughulikia dharura hiyo kwa baadhi ya watendaji wa Wizara yake. Aliahidi kuchukua hatua kali usiku wa leo, Aprili 7, 2025, ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wanaopewa majukumu ya kushughulikia masuala ya dharura na kutochukulia mambo kwa uzito unaostahili.
Hali hii imesababisha usumbufu mkubwa kwa usafirishaji wa abiria na mizigo katika njia ya kusini, na wananchi wanatarajia hatua za haraka kutoka kwa serikali ili kurejesha hali ya kawaida.