Manispaa ya Kibaha mkoani Pwani inatarajiwa kupiga hatua kubwa kimaendeleo baada ya kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 19. Fedha hizi zitatumika kujenga upya Soko kuu la Mnarani kwa mtindo wa kisasa na kuboresha miundombinu ya barabara, mradi unaolenga kubadili sura ya mji huo na kukuza uchumi wa wananchi wake.
Mradi huu umewezeshwa kupitia programu ya kimkakati ya TACTIC, inayofadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia wenye thamani ya Dola za Marekani milioni 410 (takriban TZS Trilioni 1), unaolenga kuboresha miji 45 nchini.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini na Mkandarasi DIMETOCIASA REAL HOPE LTD, Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge, alisema lengo la serikali ni kuhakikisha wananchi, hasa wafanyabiashara, wanafanya shughuli zao katika mazingira salama na ya kisasa. Alimwagiza mkandarasi kukamilisha mradi huo ndani ya miezi 15 iliyopangwa ili wafanyabiashara waweze kurejea kwenye shughuli zao haraka iwezekanavyo.
"Mradi huu ni fursa kubwa ya ajira na chanzo cha kuongeza kipato kwa wakazi wa Kibaha. Hivyo, nawasihi wananchi kuwa wazalendo kwa kulinda vifaa vya ujenzi vitakavyoletwa hapa ili kuepuka wizi unaoweza kuchelewesha mradi," alisema Kunenge.
Kwa upande wake, Mratibu Msaidizi wa Miradi ya Benki ya Dunia kutoka TAMISEMI, Mhandisi Emanuel Manyanga, alifafanua kuwa ujenzi utaanza rasmi Oktoba Mosi. Aliongeza kuwa mbali na soko na barabara, mradi utajumuisha ujenzi wa bustani ya kisasa ya mapumziko. Alisisitiza kuwa programu ya TACTIC inalenga pia kuzijengea Halmashauri uwezo wa kusimamia maendeleo ya miji na kuongeza ukusanyaji wa mapato.
Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa, kupitia kwa Pili Mnyema, imeahidi usimamizi thabiti ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa viwango vya juu. Naye Mwenyekiti wa Soko la Mnarani, Mohamed Mnembwe, ameishukuru serikali, akisema wafanyabiashara wanasubiri kwa hamu kukamilika kwa soko hilo jipya.