Mkoa wa Singida, ambao sifa yake kuu imekuwa ni uzalishaji wa alizeti na asali, sasa unazidi kujipambanua kama kitovu cha uzalishaji wa "rungu" la kiuchumi kupitia wasomi walioiva. Katika kile kinachoonekana kama mapinduzi ya elimu ya juu Kanda ya Kati, Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida, imefanya makubwa kwa kuingiza mtaani jeshi la wahitimu 1,490 huku ikijivunia mafanikio ya kishindo katika tafiti zinazolenga kumkomboa mwananchi wa kawaida kiuchumi.
Hayo yamebainishwa leo na Afisa Mtendaji Mkuu wa TIA, Profesa William Pallangyo, wakati wa sherehe za mahafali ya 23 ya taasisi hiyo tawi la Singida. Profesa Pallangyo ameweka wazi kuwa chuo hicho hakipo Singida kwa ajili ya kutoa vyeti pekee, bali kimegeuka kuwa 'maabara' ya kutatua kero za wafanyabiashara na halmashauri.
Tafiti 13: Mwarobaini wa Biashara Ndogo Profesa Pallangyo ameanika kuwa katika mwaka wa masomo 2024/2025, TIA Singida imefanikiwa kufanya tafiti na machapisho 13 yenye tija. Tafiti hizi hazikukaa maktaba na kugeuka mapambo, bali zimejikita katika kutoa majibu ya changamoto zinazowakabili wafanyabiashara wadogo na wa kati (SMEs) mkoani humo.
"Lengo letu lilikuwa ni kugusa maisha ya watu moja kwa moja. Tumetoa ushauri wa kitaalam kwa Halmashauri za Mkoa wa Singida na kutoa elimu ya usimamizi wa fedha. Tunataka kuona mama ntilie, bodaboda na wafanyabiashara wa kati wakiendesha shughuli zao kisasa na kukuza mitaji yao," alieleza Profesa Pallangyo.
Aliongeza kuwa tafiti hizo zimelenga kuimarisha sekta ya ujasiriamali na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa rasilimali fedha, jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa jamii na uchumi wa mkoa huo unaokuwa kwa kasi.
Bilioni 13.5 za Benki ya Dunia (HEET) Habari njema zaidi iliyozua shangwe katika mahafali hayo ni hatua ya serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kumwaga fedha ndefu kukiimarisha chuo hicho. Profesa Pallangyo alibainisha kuwa kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, Kampasi ya Singida imepata kiasi cha Shilingi Bilioni 13.5.
Fedha hizi zimeelekezwa katika ujenzi wa jengo jipya na la kisasa la kitaaluma. Mradi huu unatajwa kuwa utabadilisha sura ya TIA Singida na kuongeza uwezo wa kudahili wanafunzi wengi zaidi, sambamba na kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ili yaendane na soko la ajira la kimataifa.
Wahitimu 1,490 na Dira ya 2050 Akiwageukia wahitimu hao 1,490, Profesa Pallangyo aliwapa wosia mzito. Aliwakumbusha kuwa wao ni sehemu ya utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, ambayo inataka kujenga jamii yenye elimu, ujuzi na uwezo wa kujifunza.
Wahitimu hao wamepikwa na kuiva katika fani mbalimbali zinazogusa mishipa ya uchumi, ikiwemo Uhasibu, Ununuzi na Ugavi (Procurement), Biashara, Rasilimali Watu na Masoko.
"Nyinyi siyo tu watafutaji wa ajira, bali ni waundaji wa mifumo ya kiuchumi. Nendeni mkaitumie elimu ya kompyuta na taaluma zenu kuleta mageuzi kwenye ofisi na biashara mtakazozitumikia au kuanzisha," alisisitiza kiongozi huyo wa TIA.
Mahafali haya ya 23 yanaashiria ukomavu wa TIA katika kuzalisha rasilimali watu inayohitajika kusukuma gurudumu la uchumi wa viwanda na biashara nchini Tanzania.