Wizara ya Katiba na Sheria imetangaza mafanikio makubwa ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Samia Legal Aid, ambapo zaidi ya wananchi milioni mbili (2,000,000) kutoka mikoa mbalimbali nchini wamepata msaada wa kisheria tangu kampeni hiyo ilipoanza mwaka 2023.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa wizara hiyo, Ester Msambazi, aliyasema hayo wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo katika ngazi ya wilaya, uliofanyika Kata ya Malula, wilayani Arumeru, mkoani Arusha. Msambazi alieleza kuwa kampeni hiyo inaendelea kutekelezwa nchi nzima na tayari wamefika mikoa 23, huku mikoa mitatu iliyosalia ikitarajiwa kufikiwa hivi karibuni.
"Tumefanikiwa kuwafikia wananchi zaidi ya milioni mbili moja kwa moja, na pia tunatumia vyombo vya habari kuwafikia watu wengi zaidi ya wale tunaokutana nao ana kwa ana," alisema Msambazi. Aliongeza kuwa lengo kuu la kampeni ya Samia Legal Aid ni kuwasaidia wananchi wanaokabiliwa na changamoto za kisheria, hasa wale ambao hawana uwezo wa kifedha kuajiri mawakili kuwawakilisha mahakamani.
Msambazi alieleza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa upendo wake kwa wananchi, alielekeza Wizara ya Katiba na Sheria kushirikiana na wadau mbalimbali kutoa elimu kwa umma ili kuwajengea uelewa kuhusu taratibu za kisheria, haki zao, na wajibu wao.
Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Amir Mkalipa, akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Katiba na Sheria, Damas Ndumbaro, alishukuru wizara kwa kuleta kampeni hiyo kwa wananchi wa wilaya yake. Alisema kuwa kampeni hiyo inawapa wananchi fursa ya kupata elimu ya kisheria ambayo itawasaidia kutambua njia sahihi za kutafuta haki zao.
"Hii ni siku muhimu sana kwa sababu inalenga kufanikisha upatikanaji wa haki kwa wananchi waliodhulumiwa lakini hawakujua namna ya kuitafuta. Kupitia kampeni hii, wataalamu wa sheria watawasikiliza na kuwasaidia kutatua changamoto zao," alisema Mkalipa.
Kampeni ya Samia Legal Aid inaonekana kuwa na mchango mkubwa katika kuongeza uelewa wa kisheria na kuwezesha upatikanaji wa haki kwa wananchi wa Tanzania.