Akiwa ameacha nyuma umaarufu na mwangaza wa viwanja vikubwa vya mchezo wa Baseball nchini Marekani (MLB), nyota wa zamani wa timu za Boston Red Sox na Chicago Cubs, Ryan Kalish, ametua kimya kimya katika mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, akiwa na dhamira moja: kutumia muda na rasilimali zake kugusa maisha ya Watanzania wanaoishi katika mazingira magumu.
Kalish, ambaye aliwasili nchini jana, Julai 10, 2025, amesema baada ya kustaafu mchezo huo, alitafakari na kuona njia sahihi kwake ni kufanya kazi za kijamii nje ya nchi yake, ambako anaamini uhitaji ni mkubwa zaidi. Lengo lake kuu ni kutambua familia duni na kuzisaidia kuboresha makazi yao, iwe kwa kukarabati au kuzijenga upya kabisa.
Akizungumza baada ya kumpokea, Rais wa Taasisi ya New Life Foundation Tanzania, Dk. Glorious Shoo, alisema ujio wa Kalish ni funzo kubwa linaloonyesha maana halisi ya utajiri.
"Amefika mahali akaona umaarufu na kujilimbikizia mali sio jambo la msingi. Utajiri wa kweli sio wingi wa magari, nyumba, au nchi unazotembelea. Utajiri wa kweli ni umeweza kugusa maisha ya wanadamu wengine kwa kiwango gani," alisema Dk. Shoo kwa hisia.
Safari ya Kalish imepata nguvu zaidi kwa kuongozana na Shaban Chani, mwanzilishi wa shirika la "Together For Transformation" la nchini Congo DRC. Chani, ambaye ni mkimbizi aliyelelewa nchini Uganda, sasa anatumia maisha yake kusaidia watoto yatima, na amekuja Tanzania kuona namna anavyoweza kushirikiana na New Life Foundation kupanua wigo wa huduma zao.
Tayari, Kalish na Chani wameanza kutembelea baadhi ya maeneo ili kuona hali halisi na kuanza kutekeleza azma yao. Pamoja na mradi wa ujenzi wa nyumba, wapo kwenye mazungumzo na Dk. Shoo ili kuona jinsi gani wanaweza kusaidia watoto yatima nchini.
Dk. Shoo aliongeza kuwa, mbali na kazi zao za huruma, watu maarufu kama Kalish wanakuwa mabalozi wazuri wa utalii wa Tanzania, wakitangaza uzuri wa mbuga za wanyama na vivutio vingine kwa ulimwengu, na hivyo kuchangia pia katika uchumi wa nchi.