Wakati taifa likielekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, Kanisa la Waadventista Wasabato Mtaa wa Shinyanga Mjini limetuma ujumbe mzito kwa Watanzania, likiwasihi kuilinda kwa gharama zote amani ya nchi ambayo ni tunu ya thamani. Ujumbe huu ulikuwa kiini cha mahubiri yaliyohitimisha kongamano la kiroho la siku saba, maarufu kama Makambi au Sikukuu ya Vibanda, lililomalizika mwishoni mwa wiki.
Mnenaji mkuu katika makambi hayo, Mchungaji Isaya Iligo kutoka Bukoba, aliongoza maombi maalum kwa ajili ya uchaguzi ujao, akisisitiza kuwa Tanzania ni kielelezo cha umoja na mshikamano barani Afrika. Alisema, "Huwezi kujua thamani ya amani kama hujawahi kupitia uzoefu wa vita. Tusikubali kabisa tunu hii ivurugwe na mchakato wa uchaguzi. Badala yake, tuombe na tuhakikishe uchaguzi unafanyika kwa utulivu na usalama." Aliongeza kuwa ni kwa sababu ya amani iliyopo ndipo watu wanaweza kukusanyika kwa uhuru na kumuabudu Mungu, fursa ambayo haipo katika baadhi ya nchi.
Makambi hayo yaliyofanyika kuanzia Agosti 16 hadi 23, yalibeba kaulimbiu "Nitakwenda nikimtumaini Yesu." Mchungaji wa kanisa hilo la Shinyanga Mjini, Gadiel Mziray, alieleza kuwa lengo la makambi haya ya kila mwaka ni kuwakusanya waumini ili kujengwa kimaadili na kuimarisha tumaini lao kwa Mwenyezi Mungu. Alisema mafundisho waliyopata kwa siku saba yatawasaidia kuwa raia wema na watii wa sheria, jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wa jamii.
Akifafanua zaidi kuhusu asili ya ibada hiyo, Mzee Kiongozi wa Kanisa, Dk. Elison Maeja, alisema Sikukuu ya Vibanda ina misingi yake katika Maandiko Matakatifu, ambapo Mungu aliagiza watu wake wakutane kila mwaka kwa ajili ya sherehe na mafundisho maalum.
Kwa upande wa waumini waliohudhuria, Happyness Soppy, alisema kongamano hilo limemuimarisha kiimani na kumpa maarifa mapya kutokana na neno la Mungu. Sherehe hizi za Sikukuu ya Vibanda ni tukio la kila mwaka linalofanywa na makanisa ya Waadventista Wasabato kote nchini, likiwa na lengo la kuimarisha maisha ya kiroho na maadili ya jamii.