Tamasha maalum linalomkumbuka na kumuenzi Dkt. John Pombe Magufuli, ambaye anaheshimika sana kwa uongozi wake shupavu nchini Tanzania na barani Afrika, linatarajiwa kufanyika katika mataifa manne tofauti. Hafla hii si tu ya kumkumbuka kiongozi huyu, bali pia itajumuisha maombi ya pekee kwa ajili ya viongozi wengine wa Tanzania, akiwemo Rais Samia Suluhu Hassan, na kwa taifa zima. Lengo kuu ni kuombea kuendelezwa kwa sera za maendeleo ambazo zilianzishwa na Hayati Magufuli.
Mwanamuziki Arba Manillah, mwanzilishi wa taasisi ya kimataifa ya sanaa na utamaduni ya Kukaye Moto Culture yenye makao yake makuu nchini Ujerumani, ndiye mwandaaji mkuu wa tamasha hili. Akizungumzia kuhusu hafla hiyo, Manillah alimtaja Dkt. Magufuli kama ‘Mwana wa Afrika’ ambaye alijitolea kwa moyo wote kuleta maendeleo nchini Tanzania kupitia ujenzi wa viwanda na kuimarisha uchumi wa ndani kwa faida ya wananchi.
Manillah alifafanua kuwa Tamasha la Magufuli limepangwa kufanyika Machi 29 mwaka huu katika nchi ambazo taasisi yake ina matawi. Aliongeza kuwa wamefanya maandalizi ya kuwakutanisha Watanzania wanaoishi Ujerumani, Malawi, Marekani, na Tanzania pamoja na marafiki wa Tanzania katika nchi hizo.
Manillah, ambaye amewahi kutunukiwa Tuzo ya Amani nchini Ujerumani, alisema kuwa kuna mambo mengi mazuri yaliyofanywa na Dkt. Magufuli ambayo yanaendelea kuleta manufaa na yanapaswa kuenziwa na kuendelezwa. Alitolea mfano juhudi zake za kukuza matumizi ya lugha ya Kiswahili kimataifa.
Katika tamasha hilo, kutakuwa na mada mbalimbali zenye lengo la kutoa elimu na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa kuendeleza utamaduni. Mada hizo zitajikita katika lugha ya Kiswahili, historia, na urithi wa Afrika kama rasilimali muhimu kwa ajili ya kukuza uchumi wa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
“Kupitia tamasha hili, tunatoa fursa za mijadala yenye manufaa, ambayo inakuza uzalendo na heshima kwa viongozi wetu wanaofanya kazi kwa bidii kwa ajili ya Tanzania,” alisema Manillah.
Mwenyekiti wa Kukaye Moto Culture Center nchini Tanzania, Samson Karume, alisema kuwa kwa upande wa Tanzania, tamasha litafanyika katika kituo cha taasisi hiyo kilichopo Ubungo Makuburi, jijini Dar es Salaam. Alieleza kuwa tamasha hilo litatumika pia kuhamasisha vijana kujiepusha na matumizi ya dawa za kulevya na badala yake kujituma kufanya kazi katika sekta mbalimbali, ikiwemo sanaa na utamaduni.
“Kupitia kauli mbiu yake ya ‘Hapa Kazi Tu’, tunawahamasisha vijana kuangalia fursa zilizopo katika sanaa na utamaduni na kuzitumia kujipatia kipato na kuendesha maisha yao,” alisema Karume.
Aliongeza kuwa baadhi ya washiriki wanatarajia kutembelea kituo cha Kigamboni Women Sober House, ambako watakuwa na mazungumzo na wanawake wanaopokea matibabu kutokana na athari za dawa za kulevya, ambao baadhi yao ni wasanii. “Tunaamini kuwa kuwatembelea na kuzungumza nao ni sehemu ya kuwapa moyo na kuwakumbusha kuwa jamii inawahitaji warejee kwenye sanaa,” alisisitiza Karume.