Dunia ya fasihi imempoteza mmoja wa magwiji wake, Ngũgĩ wa Thiong’o, mwandishi mashuhuri na mwanaharakati wa haki za binadamu kutoka Kenya, aliyefariki dunia mwishoni mwa wiki akiwa na umri wa miaka 87 nchini Marekani. Anver Versi, mwandishi wa habari mwenye asili ya Kenya anayeishi Uingereza na aliyekuwa mwanafunzi wake miaka ya 1970, ametoa heshima zake kupitia jarida la New African, akimwelezea Ngũgĩ kama mwalimu asiye na hofu na mtetezi jasiri wa haki za watu dhidi ya ukandamizaji, ambaye pia alisisitiza uandishi wa fasihi kwa lugha za Kiafrika.
Versi anakumbuka miaka yake ya mwanzo Chuo Kikuu cha Nairobi mwanzoni mwa miaka ya 1970, ambapo Ngũgĩ alikuwa mhadhiri wake wa Fasihi ya Kiafrika. Tangu utotoni, fasihi ilikuwa shauku kubwa kwake, akifurahia kusoma vitabu kutoka Maktaba ya British Council huko Mombasa na duka dogo la vitabu vya mkononi, ambapo aliruhusiwa kuchukua vitabu bila malipo. Vitabu hivi, vilivyokuwa vimeandikwa na waandishi wa Kiingereza au Kimarekani, vilimpeleka katika walimwengu wa ajabu, ingawa mandhari yalikuwa mageni, hisia za wahusika zilimwelekea.
Kiu yake ya hadithi haikuishia hapo. Mama Andikalo, ambaye alitekwa utotoni na kuuzwa utumwani kabla ya kuokolewa na babu yake huko Zanzibar, alisimulia hadithi za Kiswahili zilizodumu kwa wiki nzima. Hadithi hizi zilihusu wahusika kama akina Ali na Masoodi, Mamadi Mkula Guniya mwenye nguvu za ajabu, Mamiya Ndege mtawala wa dunia ya ndege, na Jamila ambaye uzuri wake uliwafanya samaki waruke baharini. Pia, sinema za Kihindi zilizojaa mapenzi na misukosuko ziliongeza utajiri wa simulizi katika maisha yake.
Licha ya utajiri huu wa hadithi, Versi anasema vitabu vya shule vilijikita tu kwa waandishi wa Kiingereza kama Shakespeare na Charles Dickens, na hakukuwa na kazi za waandishi wa Kiafrika, jambo lililowafanya waamini kuwa Waafrika hawaandiki vitabu, ingawa walikuwa hodari katika kusimulia hadithi kwa mdomo. Utambulisho wake rasmi wa kwanza kwa fasihi ya Kiafrika ulitokea alipoingia Chuo Kikuu cha Nairobi. Idara ya Fasihi ya Kiingereza ilibadilishwa jina na kuwa Idara ya Fasihi tu, na Fasihi ya Kiafrika iliwekwa katikati ya mtaala. Baadaye, aligundua kuwa Ngũgĩ ndiye aliyesukuma mabadiliko haya muhimu.
Wakati huo, waandishi wachache sana wa Kiafrika walikuwa wamechapishwa, hasa kupitia Heinemann African Writers Series, ambayo ilichapisha 'Things Fall Apart' ya Chinua Achebe mwaka 1958. Waandishi kama Achebe na Wole Soyinka walikuwa wamejipatia heshima kama waasisi wa fasihi mpya, huku Afrika Mashariki ikimiliki Ngũgĩ wa Thiong’o, aliyekuwa akijulikana kama James Ngugi, ambaye riwaya zake za mwanzo ni pamoja na 'Weep Not, Child' (1964), 'The River Between' (1965), na 'A Grain of Wheat' (1967), ambazo baadhi hutumika hata katika elimu ya sekondari nchini Tanzania.
Mihadhara ya Ngũgĩ ilikuwa kivutio kikuu. Versi anakumbuka jinsi ukumbi wa mihadhara ulivyokuwa ukijaa waliposikia kuwa Ngũgĩ atafundisha 'Arrow of God' ya Achebe. Licha ya unyenyekevu wake na kimo kifupi, tofauti na matarajio ya wengi, mihadhara yake ilikuwa ya kina na isiyo na mbwembwe. Ngũgĩ aliepuka maonesho ya kihisia, akivaa shati lisilo na tai na koti la corduroy. Alianza kwa sauti ya chini, akichambua kwa kina ishara za kidini na kitamaduni katika kazi ya Achebe, wakati mwingine akitumia muda mrefu kuchambua aya moja au mbili. Hii ilifanya mihadhara yake kuwa migumu kufuata, na matokeo ya insha yalikuwa chini, isipokuwa kwa Lars, mwanafunzi kutoka Finland, ambaye alirekodi mihadhara yote na kuisikiliza kwa utulivu, jambo lililomsaidia Versi na wengine kuboresha alama zao. Ngũgĩ alikuwa mtu tofauti kabisa alipojiunga na wanafunzi kwenye 'Junior Common Room', akionyesha ucheshi na akili ya haraka.
Bila wao kujua, kulikuwa na mikondo ya chini ya kisiasa iliyokuwa ikivuma. Riwaya za mwanzo za Ngũgĩ zililenga uhusiano kati ya wakoloni na wakulima wa Kenya. Lakini mwelekeo wake ulibadilika kabisa alipoandika 'Petals of Blood' mwaka 1977, iliyoangazia kipindi cha baada ya ukoloni. Aliamini kuwa watu waliopigania uhuru walikuwa wamesalitiwa na tabaka jipya la Waafrika wenye fedha na madaraka, waliochukua nafasi ya wakoloni bila kujali maslahi ya watu wa kawaida. Kitabu hiki, riwaya ya kwanza aliyoandika kwa jina la Ngũgĩ wa Thiong’o na ya mwisho kwa Kiingereza, kilishambulia vikali tabaka la kisiasa la Kenya huru. Carey Baraka, mwandishi wa Kenya, anathibitisha kuwa Ngũgĩ, akiwa amevutiwa na Karl Marx na Frantz Fanon, alianza kujikita moja kwa moja na masuala ya dola, tabaka, elimu, na vipengele vyote vya maisha baada ya ukoloni, akionyesha elimu kama chombo kilichogeuka kuwa usaliti kwa watu.
Labda kilichomtofautisha sana Ngũgĩ na waandishi wenzake ilikuwa msimamo wake thabiti wa kukataa kabisa lugha ya Kiingereza. Wakati waandishi wengi walikiona Kiingereza kama chombo cha kuwaunganisha na kufikisha ujumbe kwa hadhira pana, Ngũgĩ aliamini kuwa haiwezekani kuondokana na fikra za kikoloni, iwapo mtu ataendelea kuandika kwa lugha ya mkoloni. Katika kitabu chake maarufu 'Decolonising the Mind', alikosoa vikali athari za lugha za kikoloni kama Kifaransa na Kiingereza katika nchi zilizowahi kutawaliwa. Msimamo wake huu ulileta mivutano hata na Chinua Achebe, mjadala unaoendelea hadi leo.
Versi anajiona mwenye bahati kuwa mwanafunzi wa mmoja wa mashujaa wake wa fasihi, akitambua kina cha uelewa wa Ngũgĩ si tu wa fasihi ya Kiafrika, bali pia wa urithi mpana wa kiutamaduni wa bara hili. Kwamba gwiji huyu wa fasihi ya dunia, ambaye mara nyingi alitarajiwa kushinda Tuzo ya Nobel, hakuwahi kutuzwa, ni miongoni mwa mifano ya wazi ya dhuluma katika historia ya tuzo hiyo. Hata hivyo, urithi wake utaishi milele, na vita aliyoiwasha ya kutafuta haki bado inaendelea. Pumzika kwa amani, Ngũgĩ wa Thiong’o.