Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, ametoa heko kwa Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Shinyanga, akipongeza jitihada zao za kutekeleza miradi ya maji inayowezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijijini. Pongezi hizi zimetolewa wakati wa uzinduzi rasmi wa mradi mkubwa wa maji uliotekelezwa katika vijiji vya Chona, Ubagwe, na Bukomela vilivyopo Halmashauri ya Ushetu, wilayani Kahama.
Ussi amesema kwamba utekelezaji huu wa miradi ya maji ni uthibitisho wa ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kufikisha huduma muhimu za maji hadi maeneo ya vijijini. "Tunaona ahadi ya Rais Samia ikitekelezwa kwa vitendo. RUWASA mmefanya kazi nzuri, mmemheshimisha Rais na mnastahili pongezi," alisema Ussi.
Akionyesha kuridhishwa na utekelezaji wa mradi, kiongozi huyo amebainisha kuwa baada ya ukaguzi wa kina wa mradi pamoja na nyaraka zake zote, Mwenge wa Uhuru umejiridhisha kuwa mradi umetekelezwa kwa viwango na hauna dosari yoyote. Ametoa pongezi za pekee kwa Meneja wa RUWASA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi Julieth Payovela na timu yake kwa usimamizi mzuri.
Akitoa taarifa ya mradi, Meneja wa RUWASA wilaya ya Kahama, Mhandisi Maduhu Magili, alieleza kuwa kabla ya utekelezaji wa mradi huu, vijiji hivyo vitatu vilikuwa na changamoto kubwa ya ukosefu wa maji kwa muda mrefu. Ujenzi wa mradi huu ulianza Februari 14, 2024 na kukamilika Julai 28, 2025, ukitumia vyanzo vitatu vya maji kutoka visima virefu vilivyochimbwa katika maeneo husika. Jumla ya Shilingi bilioni 1.4 zimetumika katika kufanikisha mradi huu.
Mhandisi Magili alisema mradi huo umenufaisha kaya 961, zenye wakazi wapatao 5,763 ambao sasa wanapata maji safi. Tayari, zaidi ya wateja 20 wameunganishiwa huduma ya maji safi majumbani mwao. Kwa upande wao, wananchi wa vijiji hivyo walionyesha furaha kubwa, wakieleza kuwa mradi huo umewaondolea adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji, na sasa wanatumia maji safi kwa shughuli zao za kila siku. Hili ni hatua kubwa katika kuboresha afya na maisha ya wananchi vijijini.