Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imefanikisha kwa mara ya kwanza kufanya upasuaji wa upandikizaji wa marejeo wa viungo vya nyonga na magoti kwa wagonjwa saba. Upasuaji huu ulifanyika katika kambi maalum iliyoandaliwa kwa muda wa siku nne, kuanzia tarehe 14 hadi 17 Aprili, 2025.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam wakati wa kambi hiyo, Mkurugenzi wa Huduma za Upasuaji wa hospitali hiyo, Dk. Godlove Mfuko, alieleza kuwa tangu kuanza kwa huduma za upasuaji wa kubadilisha nyonga na magoti kwa kutumia vifaa bandia mwaka 2022, zaidi ya wagonjwa 275 wamekwisha kupata matibabu haya muhimu.
Dk. Mfuko aliongeza kuwa katika kliniki ya mifupa ya hospitali hiyo, matatizo yanayohusu nyonga na magoti yanashika nafasi ya pili kwa wingi wa wagonjwa wanaohudumiwa, yakifuatia kwa karibu matatizo ya mgongo. Takwimu zinaonyesha kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Machi mwaka 2025, hospitali ilihudumia wagonjwa 4,513 katika kliniki hiyo, na kati yao, 1,527 walikuwa wakisumbuliwa na matatizo ya nyonga na magoti.
“Hii ni sawa na asilimia 34 ya wagonjwa wote tuliowaona katika kipindi hicho. Kwa wastani, kwa kila mwezi tunapokea kati ya wagonjwa 450 hadi 550 wenye matatizo haya. Tumekuwa tukishirikiana na hospitali mbalimbali nchini, kama vile Hospitali ya Temeke na Hospitali ya CCBRT, katika kutoa huduma hizi,” alisema Dk. Mfuko.
Alifafanua kuwa hapo awali, upasuaji wa marejeo ya nyonga na magoti haukuweza kufanyika nchini kutokana na uhaba wa wataalamu wenye ujuzi maalum pamoja na ukosefu wa vifaa vya upandikizaji wa marejeo. Hata hivyo, sasa hospitali imewezesha upatikanaji wa huduma hii, na upasuaji huo utakuwa endelevu kwa wagonjwa wanaohitaji.
“Matibabu haya ni sehemu ya mkakati wa serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan wa kupeleka huduma bobezi karibu na wananchi. Tumefanya upasuaji huu kwa ushirikiano wa karibu na wataalamu kutoka nchini China, ambao wana uzoefu mkubwa katika upasuaji huu,” alibainisha Dk. Mfuko.
Alieleza zaidi kuwa gharama za matibabu kwa mtu mmoja anayekwenda kutibiwa nje ya nchi kwa ajili ya upasuaji huu ni takriban Shilingi milioni 27 za Kitanzania, wakati gharama ndani ya nchi ni Shilingi milioni 13.5. Hii inaonyesha wazi kuwa kufanyika kwa upasuaji huu nchini kutapunguza kwa kiasi kikubwa mzigo wa gharama kwa wagonjwa na taifa kwa ujumla.
“Kwa bahati mbaya, bado hatuna utaratibu wa bima kwa ajili ya matibabu haya. Hata hivyo, tutakaa na wenzetu wa kampuni za bima ili kujadili namna ya kuingiza huduma hii muhimu katika vifurushi vyao vya bima ili wananchi wengi zaidi waweze kumudu gharama,” aliongeza.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa Bobezi wa Upasuaji wa Nyonga na Magoti, Dkt. Shilekirwa Makira, alieleza kuwa sababu kuu za kusagika kwa mifupa ya nyonga na magoti mara nyingi zinatokana na masuala ya kimaumbile.
“Kuna watu ambao kadiri umri unavyosonga, wanaweza kupata changamoto hii. Sababu nyingine ni magonjwa kama vile ugonjwa wa baridi yabisi (osteoarthritis), ambao mtu anaweza kuwa nao tangu akiwa mdogo. Pia, ajali, hasa zile zinazotokea katika umri mdogo na kusababisha mifupa kutorekebishwa vizuri, zinaweza kuchangia tatizo hili baadaye,” alisema Dkt. Makira.
Aliongeza kuwa ugonjwa huu unawaathiri zaidi watu wenye umri kuanzia miaka 60 na kuendelea, pamoja na watu wanaougua ugonjwa wa selimundu.
“Mara ya kwanza unapofanyiwa upasuaji wa kubadilisha nyonga au goti, vifaa hivyo vinaweza kudumu kwa miaka 20 hadi 25. Ikitokea changamoto yoyote, kama vile kuharibika au kuambukizwa, mgonjwa analazimika kufanyiwa upasuaji wa marejeo. Pia, wale wanaopata ajali baada ya upasuaji wa kwanza wanaweza kuhitaji upasuaji wa marejeo,” alifafanua.
Dkt. Makira aliwashauri wananchi kufanya uchunguzi wa mapema kwa madaktari ili waweze kupewa virutubisho vinavyoweza kuchelewesha mchakato wa kusagika kwa magoti na nyonga. Pia, aliwaasa wale ambao wamekwisha kufanyiwa upasuaji kuzingatia maelekezo yote ya matibabu ili kuepuka kupata maambukizi ambayo yanaweza kuharibu matokeo ya upasuaji.
Mmoja wa madaktari kutoka Hospitali ya Macho ya CCBRT walioshiriki katika kambi hiyo ya upasuaji, Dk. Prosper Alute, alishukuru Hospitali ya Mloganzila kwa hatua hiyo muhimu, akisema kuwa upasuaji wa kwanza wa kubadilisha nyonga na magoti unafanyika kwa kiasi kikubwa, lakini upasuaji wa marejeo umekuwa ukifanyika kwa nadra sana.
“Tunaamini tutaendelea kujifunza kutoka kwa madaktari wengine wenye uzoefu, na hatimaye tutaweza kuanza kutoa huduma hizi za upasuaji wa marejeo katika vituo vyetu vya CCBRT,” alimalizia Dk. Alute.