Mkuu wa Wilaya Atoa Eneo kwa Ajili ya Upandaji Miti Shule ya Shadi, Kampuni ya The Guardian Yatoa Miti

culture | Thu May 22 2025


Mkuu wa Wilaya Atoa Eneo kwa Ajili ya Upandaji Miti Shule ya Shadi, Kampuni ya The Guardian Yatoa Miti

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi, ametoa eneo ndani ya shule mpya ya msingi ya Shadi, iliyoko katika Kata ya Luchelele jijini Mwanza, kwa ajili ya kupandwa na kutunzwa miti iliyotolewa na Kampuni ya The Guardian Ltd.


Kati ya miti 2,000 iliyoahidiwa, kampuni hiyo tayari imetoa miti 200 ambayo imepandwa katika shule hiyo. Hii inaongeza juhudi zilizokuwa zimefanywa awali ambapo miti iliyotolewa na serikali kupitia ahadi ya Tuzo ya Mwandishi Mahiri wa Habari za Mazingira, iliyopandwa katika shule ya msingi ya Luchelele, ilikuwa imeshaanza kukua.


Akizungumza wakati wa kutoa eneo hilo, Mkuu wa Wilaya alipongeza kampuni ya The Guardian Ltd kwa kuonyesha mfano wa kuunga mkono juhudi za serikali katika uhifadhi wa mazingira, akiongeza kuwa hatua yao inaongeza nguvu katika kile ambacho tayari kimefanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan.


Aidha, aliiomba kampuni hiyo, kupitia wawakilishi wake waliopo jijini humo, akiwemo mshindi wa Tuzo hiyo, Vitus Audax, kuwa sehemu ya kufuatilia na kuhakikisha miti iliyopandwa inatunzwa vizuri na kufikia malengo yaliyokusudiwa.


Akizungumza baada ya upandaji wa miti hiyo, Vitus Audax alisema kuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya The Guardian Ltd ametoa miti hiyo kama sehemu ya kurudisha sehemu ya faida kwa jamii, ikiwa ni kuunga mkono kile ambacho serikali imekifanya kupitia mshindi wa Tuzo ya Samia Kalamu Awards katika masuala ya mazingira.


"Tayari tumekabidhi na kupanda miti 200 katika eneo hili, ikiwemo miti ya matunda kama parachichi na mipera, pamoja na miti ya kutoa kivuli na mbao. Hii inaongeza ile miti ambayo tayari serikali ilitoa na tulipanda katika shule ya msingi ya Luchelele," alisema Vitus Audax.


Aliongeza kuwa kampuni hiyo inatarajia kutoa miti mingine 1,800 hivi karibuni, ambayo itakabidhiwa kwa ofisa misitu wa Jiji la Mwanza. Lengo kuu ni kuendeleza kampeni ya kufikia lengo la kupanda miti milioni 1.5 jijini humo, kama sehemu ya juhudi za kulinda na kuhifadhi mazingira kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.