Maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2025 yamepangwa kufanyika kitaifa kuanzia Juni 16 hadi Juni 23, 2025, katika viwanja vya Chinangali jijini Dodoma. Lengo kuu la maadhimisho haya ni kutambua na kuthamini mchango mkubwa wa watumishi wa umma katika kuleta maendeleo endelevu ya taifa.
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dodoma, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi, alieleza kuwa maadhimisho hayo yataambatana na maonesho mbalimbali. Maonesho haya yanalenga kuwawezesha watumishi wa umma kufahamu kwa undani dira, dhima, malengo, programu, mikakati, mafanikio yaliyopatikana, na changamoto zinazoikabili sekta ya utumishi wa umma.
"Maadhimisho haya pia yanalenga kuwahamasisha na kuwapa motisha watumishi wa umma kuendelea kufanya kazi yao vizuri katika ujenzi wa taifa. Tunataka waendelee kuwa wabunifu katika kutafuta suluhu za changamoto mbalimbali zinazoikumba jamii yetu," alisema Katibu Mkuu Mkomi. Aliongeza kuwa maadhimisho hayo yatatoa fursa ya kupata mrejesho muhimu kutoka kwa wananchi na wadau wanaopokea huduma kutoka kwa watumishi wa umma. Mrejesho huu utasaidia kuandaa utumishi wa umma ili uweze kukabiliana na changamoto za baadaye kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu.
Bwana Mkomi alieleza kuwa wananchi watafaidika kwa kupata uelewa mzuri wa wajibu wao na haki zao. Uelewa huu utawawezesha kujua namna ya kudai haki zao pale wanapozikosa. Aidha, taasisi za umma zitapata fursa muhimu ya kubadilishana uzoefu kuhusu mbinu na mikakati mipya ya kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.
"Katika maonesho haya, wananchi wataweza kupata huduma mbalimbali papo kwa hapo. Huduma hizo ni pamoja na upatikanaji wa vyeti vya kuzaliwa, vitambulisho vya taifa (NIDA), hati za viwanja, na huduma za kupima afya zinazotolewa na wataalamu kutoka Hospitali za Benjamin Mkapa, Taasisi ya Jakaya Mrisho Kikwete (JKCI), Hospitali ya Taifa Muhimbili, na Taasisi ya Mifupa (MOI). Pia, kutakuwepo na huduma ya kupata Gazeti la Serikali," alifafanua Katibu Mkuu.
Maadhimisho haya yanatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano kati ya watumishi wa umma na wananchi, na pia kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma za umma nchini Tanzania.