Mkoa wa Shinyanga, ardhi maarufu kwa utajiri wa madini na utamaduni wa Kisukuma, hivi sasa unapita katika kipindi kigumu cha 'kulipa kisasi' cha asili. Ikiwa imesalia siku chache tuuage mwaka 2025, hali ya hewa katika mkoa huu imebadilika na kuwa tishio kwa usalama wa maisha na mali za wananchi, jambo linaloashiria kuwa mabadiliko ya tabianchi si hadithi za kwenye vitabu tena, bali ni uhalisia unaoishi nasi.
Ripoti za kusikitisha kutoka Wilayani Kahama na Shinyanga zinaeleza kuwa mnamo Desemba 12, 2025, "gadhabu ya asili" ilishuka kwa kishindo. Mvua kubwa iliyoambatana na upepo mkali—kama wa kisulisuli—ilisababisha maafa makubwa ambapo zaidi ya nyumba 200 ziliangushwa, na kuacha mamia ya familia bila pa kujishikiza. Katika tukio la kuhuzunisha zaidi wilayani Shinyanga, mtu mmoja alipoteza maisha baada ya kuangukiwa na ukuta, tukio ambalo limeacha simanzi nzito.
DC Mtatiro: "Nchi Ipo Uchi"
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Komredi Julius Mtatiro, hakumung'unya maneno alipozungumzia janga hili. Kwa uchungu, aliweka wazi kuwa maafa haya ni matokeo ya wananchi 'kuivua nguo' ardhi kwa kukata miti ovyo, na kuiacha nchi ikiwa na 'kipara'.
"Chanzo kikubwa cha maafa haya ni maeneo mengi kuwa wazi bila miti. Desemba 12, upepo ulikosa kizuizi, ukapiga kwa kasi na kuangusha nyumba. Hii ni kengele ya hatari," alisisitiza Mtatiro.
Kauli ya DC Mtatiro inaungwa mkono na ushuhuda wa Bwana Jilala Duttu, mkazi wa Ibanza ambaye ni mmoja wa wahanga. Akisimulia kwa hisia, Duttu alisema ilipofika saa tisa usiku, alisikia kishindo cha upepo ambacho hakujawahi kukisikia, na ghafla mabati yalianza kupaa kama tiara.
"Hali ilikuwa ya kutisha. Nyumba ilianguka, mtoto wangu akajeruhiwa kwa tofali kichwani na mama mkwe aka-vunjika mguu. Tunamshukuru Mungu uhai upo, lakini mali zimepotea," alisimulia Duttu kwa masikitiko.
Vita Dhidi ya Mkaa na Utamaduni wa Ufugaji
Changamoto kubwa Shinyanga si kupanda miti pekee, bali 'kuilea'. Takwimu kutoka kwa Ofisa Mazingira wa Manispaa, Ezra Manjerenga, zinaonyesha kuwa kati ya Julai 2024 na Juni 2025, miche 994,213 ilipandwa. Hata hivyo, zaidi ya miti 208,000 'ilifia njiani'. Sababu? Mifugo kuachwa ichunge hovyo na ukosefu wa utunzaji. Hii ni changamoto ya kiutamaduni ambapo ufugaji holela unageuka kuwa adui wa mazingira.
Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) nao wameingia vitani. Fabian Balele, Ofisa Mwandamizi wa TFS Shinyanga, amebainisha kuwa biashara ya mkaa ndio "mzizi wa fitina." Kila siku, watu sita hadi saba wanatiwa mbaroni kwa biashara hii haramu.
"Lakini hatuishii kukamata tu. Mwaka 2026, TFS Shinyanga tutaleta mapinduzi kwa kuleta mashine za kuzalisha mkaa mbadala usiotokana na miti. Tutatoa mafunzo bure ili wananchi waachane na kukata miti," aliahidi Balele, huku akisisitiza kuwa TFS inagawa miche milioni moja kila mwaka, ikiwemo miche 600,000 iliyogawiwa bure mwaka huu.
Tanzania Kung'ara COP30 Brazil
Wakati Shinyanga ikipambana na hali halisi, Tanzania inazidi kupaza sauti kimataifa. Dk. Richard Muyungi, Mwenyekiti wa Kundi la Afrika la Majadiliano (AGN), ameleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika mkutano wa COP30 huko Belem, Brazil. Tanzania imeweza kuingiza wataalamu sita kwenye kamati nyeti za maamuzi ya dunia.
Hii ni hatua kubwa katika kusukuma ajenda ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya Nishati Safi ya Kupikia (NCCS 2024–2034), ambayo inalenga kuhakikisha asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ifikapo 2034. Mkakati huu ndio mwarobaini pekee utakaookoa miti ya Shinyanga na kuzuia maafa ya nyumba kuanguka siku za usoni.