Katika kile kilichoonekana kama utabiri wa kiroho uliopambwa na uhalisia wa kisayansi, Mhashamu Baba Askofu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, ametoa ujumbe mzito kwa Watanzania wakati wa Misa ya Mkesha wa Noeli, akiwataka kujiandaa kiimani kwa mwaka 2026 ambao ametabiri utakuwa na changamoto zake, hasa za kimazingira.
Akihubiri kutoka katika madhabahu ya Parokia ya Mtakatifu Paulo wa Msalaba iliyopo jijini Dodoma, Makao Makuu ya Nchi, kiongozi huyo wa kiroho aliwataka waumini kumfanya Kristo kuwa "jirani na rafiki wa kudumu" ili kuweza kuhimili mawimbi ya kimaisha yanayotarajiwa.
Tahadhari ya Tabianchi na Mwaka 2026
Katika hali isiyo ya kawaida, Askofu Kinyaiya hakumung'unya maneno kuhusu mabadiliko ya tabianchi yanayoikabili dunia na Tanzania kwa ujumla. Aligusia hali ya joto kali inayoshuhudiwa sasa kama ishara ya mambo yajayo.
"Tunaona sasa hivi kuna mabadiliko makubwa ya tabianchi, tunapata joto sana. Mwaka 2026 utakuwa na changamoto, huenda usiwe mzuri sana kimazingira," alionya Askofu huyo, huku akisisitiza kuwa njia pekee ya kupata faraja katikati ya 'joto' hilo la kimaisha ni kumkimbilia Mtoto Yesu aliyezaliwa.
Ujumbe Mahususi kwa "Wababa" na Familia
Katika kugusa mzizi wa utulivu wa familia, Askofu Kinyaiya aligeukia upande wa akina baba, akitoa agizo la kiubaba linalolenga kuimarisha upendo ndani ya nyumba. Alikemea tabia ya baadhi ya wanaume kuacha familia zao wakati wa sikukuu na kwenda kufurahia maisha na marafiki au 'kujirusha' baa.
"Naomba akina baba mkae nyumbani kwenu. Ukae nyumbani watoto wakuone, wajue baba yupo. Hizo safari za kwenda kutembea kwa rafiki zako zipange siku nyingine, lakini hii ni siku maalum ya familia," alisisitiza kwauonjo wa upendo.
Kioo cha Matatizo ya Jamii ya Sasa
Mhashamu Askofu alitumia fursa hiyo kuchambua kwa kina 'misalaba' inayowatesa Watanzania wengi hivi leo. Alilinganisha kuzaliwa kwa Yesu katika zizi la ng'ombe—sehemu ya harufu mbaya na duni—na hali ngumu wanazopitia wananchi wa kawaida.
Alisema, "Nimejiuliza kwanini Mungu alitaka Yesu azaliwe hivyo? Jibu ni kwamba alitaka tujifananishe naye." Askofu aliorodhesha changamoto zinazoumiza vichwa vya wengi mitaani zikiwemo:
- Majungu na Kijicho Kazini: Watu kusemana na kuharibiana sifa sehemu za kazi.
- Migogoro ya Ndoa: Mivutano kati ya wanandoa, au baina ya wakwe na mawifi.
- Uchumi na Madeni: Watu kudaiwa na kukosa pesa za sikukuu, au wale wenye pesa kugoma kulipa madeni yao kwa makusudi.
- Kuchelewa Kuolewa: Mabinti wanaosubiri waume bila mafanikio.
Kutokana na uzito wa matatizo haya, Askofu Kinyaiya alikemea vikali wimbi la watu kukata tamaa hadi kufikia hatua ya kujitoa uhai. "Watu wengine wanaamua kujinyonga kwa sababu hawana imani. Tusimuache Yesu, tumtegemee atatusaidia kutatua changamoto zetu badala ya kukatisha uhai," aliusia.
Wito wa Ukarimu
Mwisho, alihitimisha kwa kuwakumbusha kuwa sherehe za Noeli si za kula na kunywa pekee, bali ni "vitega uchumi vya neema" kupitia kuwasaidia wahitaji. Aliwahimiza waumini kutembelea wagonjwa, yatima, na wafungwa magerezani, akisema kuwa hao ndio daraja la kupata baraka kutoka kwa Mungu.
Misa hiyo iliyopambwa na nyimbo za shangwe, iliadhimishwa kwa ushirikiano na Padri Beno Mganga, Paroko wa Parokia hiyo, pamoja na Padri Saimon Swaga, huku waumini wakionekana kuguswa na ujumbe huo uliochanganya uhalisia wa maisha ya Mtanzania na imani.