Katika kile kinachoweza kutajwa kama 'mkono mrefu wa sheria' kufanya kazi yake bila kigugumizi, Mahakama mkoani hapa imetoa fundisho kali kwa wahalifu baada ya kumhukumu Bwana Yaledi Sinkala (38), mkazi wa Wilaya ya Momba, kifungo kizito cha miaka 40 jela. Hukumu hiyo imekuja baada ya mtuhumiwa huyo kutiwa hatiani kwa kosa la kinyama la kufanya mapenzi na maharimu wake (ndugu wa damu) ambaye ana changamoto ya afya ya akili.
Tukio hilo ambalo limeacha simanzi na mshangao kwa wakazi wa Momba, limechukuliwa kama onyo kali kwa wale wenye tabia za kinyama za kutumia udhaifu wa wengine, hususan wenye ulemavu, kukidhi matamanio yao ya kimwili.
Jeshi la Polisi Lawasha Moto
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo, Desemba 24, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe (RPC), Augostino Senga, amebainisha kuwa hukumu hiyo ilitolewa Novemba 18, 2025 katika Mahakama ya Wilaya, baada ya jeshi hilo kukamilisha upelelezi na kuwasilisha ushahidi usio na shaka.
"Kitendo alichofanya Yaledi ni cha aibu, ni kinyume na utu, na ni kinyume na sheria za nchi. Mahakama imeona inafaa kumpa adhabu hiyo ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye nia ovu kama hii," alisema Kamanda Senga huku akisisitiza kuwa Songwe siyo kichaka cha wahalifu.
Orodha ya Walioiona 'Cha Moto'
Katika mkutano huo ulioangazia mafanikio ya jeshi hilo katika kudhibiti uhalifu, Kamanda Senga hakumtaja Yaledi pekee. Amebainisha kuwa operesheni kabambe inayoendelea mkoani humo imeweza kuwatia nguvuni wahalifu wengine sugu ambao tayari wamesahau uraia wa mtaani na kuanza maisha mapya gerezani.
Mmoja wao ni Nyati Kapongo (32), mkazi wa Wilaya ya Songwe, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kubaka. Hukumu hii ilitolewa Novemba 24, 2025, ikiwa ni ishara kuwa vita dhidi ya ukatili wa kijinsia mkoani humo inapiganwa kwa vitendo na si maneno matupu.
Vilevile, "mkono wa chuma" umemwangukia Bwana Walless Mwamengo (45), ambaye amekutwa na hatia ya uhujumu uchumi. Mahakama ya Wilaya ya Songwe imemhukumu kifungo cha miaka 20 jela pamoja na kumlipa faini ya Shilingi Milioni 7 (TZS). Hii ni baada ya kesi yake kutolewa maamuzi mnamo Novemba 19, 2025.
Ulinzi wa Sikukuu: "Hakuna Kulala"
Akigeukia suala la usalama kuelekea kilele cha sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya, Kamanda Senga ametangaza "hali ya hatari" kwa wahalifu wote. Amesema Jeshi la Polisi Songwe limejipanga vilivyo kuhakikisha wananchi wanakula sikukuu kwa amani na utulivu.
"Tumeimarisha ulinzi kila kona. Kuanzia kwenye nyumba za ibada, kumbi za starehe, viwanja vya michezo ya watoto, hadi mitaani kwenye makazi ya watu. Doria zetu zitahusisha magari, pikipiki, askari wa miguu, na kikosi maalum cha mbwa wa polisi ili kunusa uhalifu kabla haujatendeka," alieleza Kamanda huyo kwa kujiamini.
RPC Senga amehitimisha kwa kuwaomba wananchi wa Mkoa wa Songwe kuwa "polisi jamii" kwa kutoa taarifa za haraka pindi wanapoona viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani, akiamini kuwa ushirikiano ndiyo silaha pekee ya kuufanya mkoa huo kuwa salama wakati wote.