DC Nyamwese Atoa Onyo Kali Handeni: 'Vishikwambi si vya Instagram na Youtube, ni vya Kuhesabu Ng'ombe'

culture | Mon Sep 22 2025


DC Nyamwese Atoa Onyo Kali Handeni: 'Vishikwambi si vya Instagram na Youtube, ni vya Kuhesabu Ng'ombe'

Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, ametoa onyo kali kwa Maofisa Mifugo wa Halmashauri ya Mji Handeni, akiwataka kutumia vishikwambi (tablets) walivyokabidhiwa na serikali kwa madhumuni ya kazi pekee na si kwa starehe za mitandaoni. Onyo hilo lilitolewa Septemba 22, 2025, wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa hivyo 25 vilivyotolewa na serikali ili kurahisisha zoezi la utambuzi wa mifugo wilayani humo.


Akizungumza kwa msisitizo, Nyamwese alisema vifaa hivyo vya kielektroniki ni zana za kazi zenye lengo la kuongeza ufanisi na si kwa matumizi binafsi. "Hivi vishikwambi vimenunuliwa ili kuharakisha utambuzi wa mifugo na kuboresha huduma kwa wafugaji. Tusije tukasikia vimeanza kutumika kuperuzi Instagram, Facebook, YouTube au kufanya 'Live Stream'. Hilo halikubaliki kabisa," alionya Mkuu huyo wa Wilaya.


Aliongeza kuwa endapo kifaa chochote kitapata hitilafu, ni lazima kipelekwe kwenye Kitengo rasmi cha TEHAMA cha Halmashauri kwa ajili ya matengenezo, na si kwa mafundi wa mitaani ambao wanaweza kuharibu mfumo wake.


Kwa upande wake, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Aldegunda Matunda, alieleza umuhimu wa vifaa hivyo akibainisha kuwa Halmashauri ina maofisa 27 tu wanaohudumia wafugaji takriban 34,484 wenye jumla ya mifugo zaidi ya 148,000. Alisema kabla ya kupokea vishikwambi hivyo 25, walikuwa na viwili pekee, hali iliyokwamisha kasi ya zoezi la utambuzi.


"Hadi sasa, utambuzi wa ng'ombe umefikia asilimia 58 na mbuzi ni asilimia 17 tu. Tunaamini kwa msaada huu wa vifaa vya kisasa, tutakamilisha zoezi hili kwa haraka na kwa ufanisi zaidi," alisema Matunda. Vifaa hivi vinatarajiwa kuleta mapinduzi katika ukusanyaji wa takwimu na usimamizi wa sekta ya mifugo katika Halmashauri ya Mji wa Handeni.

I recommend this article.

You can participate in article recommendations up to 50 times within 24 hours.


0 comments


Messages unrelated about this certain topic may be deleted or restricted.

0/300
Loading...

The copyright for this content belongs to the copyright holder or provider. Unauthorized use may result in legal liability under copyright laws and other regulations.