Mkuu wa Wilaya ya Mbogwe, Sakina Mohamed, amewataka wazazi na walezi kote nchini kutambua jukumu lao la msingi katika malezi sahihi ya watoto, na kuwakumbusha kuepuka kupita kiasi katika kuwapenda kwani kunaweza kuharibu maisha ya baadaye ya watoto wao. Akizungumza kwenye mahafali ya 13 ya Shule ya Msingi Waja Springs iliyopo Manispaa ya Geita, Sakina alisisitiza umuhimu wa malezi ya nyumbani kwenda sambamba na mafunzo wanayopata watoto shuleni. Alieleza kuwa ushirikiano huu wa malezi ndiyo unaowawezesha watoto kujitambua na kujiamini katika maisha.
Sakina pia alitoa tahadhari kali kwa wazazi dhidi ya matumizi mabaya ya teknolojia, hasa simu za mkononi na televisheni. Alisema kuwa zimechangia pakubwa katika mabadiliko ya tabia za watoto, na kuwataka wazazi kuwa macho na kuchunguza kila mara aina ya maudhui ambayo watoto wao wanatazama kwenye mitandao ya kijamii. Alisisitiza kuwa, hata kama wazazi wana shughuli nyingi, haipaswi kuwa kisingizio cha kupuuza malezi. Watoto wasipopata mwongozo sahihi, hawatakuwa na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.
Aliongeza kuwa malezi ni jukumu la pande zote mbili, nyumbani na shuleni. Alisisitiza kuwa upendo kupita kiasi huweza kumharibu mtoto na kumfanya ashindwe kukabiliana na maisha halisi. Kwa mujibu wake, hata kama mwalimu amemfundisha mtoto kwa miaka saba akiwa na nidhamu, kipindi anachokaa nyumbani kabla ya kuanza masomo ya sekondari ni muhimu zaidi kwani ndicho kinachomjenga na kumwandaa kwa maisha yajayo.
Nasooro Salum, mmoja wa wazazi waliohudhuria mahafali hayo, alishauri kuwa, katika kipindi hiki cha utandawazi, ni bora watoto waangalie televisheni badala ya simu, na kwamba vipindi vinavyooneshwa kwenye runinga vikaguliwe kwanza. Alisisitiza kwamba wazazi wanapaswa kuweka mipaka ya wazi kwa watoto wao, kwa kutumia maneno ‘ndiyo’ na ‘hapana’ pale inapohitajika. Alisema ukali wa kiasi unahitajika ili kuwajenga watoto wenye maadili mema na heshima.