Mtambo (Bulldozer) unaomilikiwa na kampuni ya uchimbaji madini ya dhahabu ya Bucreef umeparamia nyumba na kusababisha majeraha kwa watu watano na kuharibu nyumba tatu katika Kitongoji cha Isangiro, Kata ya Rwamgasa, Wilaya ya Geita, Mkoa wa Geita.
Akizungumzia tukio hilo lililotokea Aprili 3, 2025, Mkuu wa Wilaya ya Geita, Hashim Komba, alisema kuwa dereva wa mtambo huo aliruka kutoka kwenye mtambo na kuuacha ukiendelea kusonga mbele kwa umbali wa kilomita moja, na hivyo kusababisha madhara hayo.
Kiongozi huyo, ambaye alifika eneo la tukio, alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa dereva aliyekuwa akiuendesha mtambo huo alikuwa anajihusisha na wizi wa mafuta. Alipogundua kuwa anafuatiliwa, aliamua kuuacha mtambo na kukimbia kusikojulikana.
Kwa mujibu wa Komba, mwendeshaji wa mtambo huo alikuwa anashirikiana na watu wengine wawili katika wizi huo wa mafuta. Baada ya watu wa mgodi kugundua wizi huo, dereva alianza kuondoka na alipogundua kuwa anafuatiliwa, aliruka kutoka kwenye mtambo.
"Usiku wa saa nane, mtambo huo uliparamia nyumba za wananchi wakiwa wamelala, ukavunja kuta. Kupona kwa watu hao ilikuwa ni muujiza wa Mungu," alisema Komba.