Mkazi mzee wa Mtaa wa Kambi Tano, Kata ya Lukobe, Manispaa ya Morogoro, Bi. Rahma Widawe (70), amejikuta akipata hifadhi katika Msikiti wa Al-Rahiminyap baada ya nyumba yake ya vyumba vitatu kubomolewa na watu wanaodai kuwa wana amri kutoka mahakamani.
Tukio hilo la kusikitisha liliambatana na uwepo wa polisi wenye silaha, ambao walisimamia zoezi la ubomoaji huo.
Akizungumza na Nipashe Digital, Bi. Widawe alieleza kuwa Machi 11, 2025, majira ya saa 8 mchana, alipokuwa nyumbani kwake, walifika watu waliokuwa wameongozana na askari wenye bunduki. Alisema watu hao walijitambulisha kuwa ndio wamiliki halali wa eneo hilo na nyumba iliyokuwa imejengwa, na wakaanza kuvunja nyumba yake kwa kutumia nyundo na miti.
Bi. Widawe alifafanua zaidi kuwa awali aliitwa katika Mahakama ya Wilaya ya Morogoro, ambapo alidaiwa kuwa amevamia eneo ambalo alijenga nyumba yake. Eneo hilo inadaiwa kuwa ni mali ya mtu mwingine aliyepata hati kutoka manispaa.
"Kesi ilisikilizwa, lakini wakati mwingine sikuwepo kwa sababu naumwa mara kwa mara. Wakati mwingine naanguka na kupoteza fahamu hata kwa siku tatu hadi tano na kupoteza kumbukumbu. Sikuweza kuhudhuria mahakamani. Naomba serikali inisaidie," alisema Bi. Widawe kwa masikitiko makubwa.
Mmoja wa mashuhuda wa ubomoaji huo, Bi. Hadija Abdalah, alieleza kuwa alishuhudia polisi wenye bunduki, na kwa maoni yake, kitendo hicho dhidi ya bibi mzee huyo ni ukatili mkubwa.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kambi Tano, Bwana Eliamini Kimaro, alieleza kushangazwa na tukio hilo na kusema kuwa mmiliki wa nyumba hakupewa nafasi ya kuokoa mali zake, kama vile matofali, mabati, na samani nyingine.